TIMU ya Austria imefanikiwa kufuzu Hatua ya 16 Bora Kombe la Mataifa ya Ulaya ‘Euro 2024’ baada ya ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Uholanzi katika mchezo wa mwisho wa Kundi D usiku wa Jumanne Uwanja wa Olympia Jijini Berlin nchini Ujerumani.
Mabao ya Austria yalifungwa na mshambuliaji wa Donyell Malen aliyejifunga dakika ya sita na viungo, Romano Schmid wa Werder Bremen, dakika ya 59 na Marcel Sabitzer wa Borussia Dortmund dakika ya 80.
Kwa upande wao Uholanzi mabao gao yalifungwa na winga wa Liverpool, Cody Gakpo dakika ya 47 na mshambuliaji wa Atlético Madrid, Memphis Depay dakika ya 75.
Mechi nyingine ya mwisho ya Kundi D Ufaransa ilitoa sare ya kufungana bao 1-1 na Poland Uwanja wa Westfalen Jijini Dortmund.
Mabao yote yalipatikana kwa penalti na yakifungwa na Manahodha na washambuliaji, nyota mpya wa Real Madrid, Kylian Mbappé mwenye asılı ya Cameroon akianza kuifungia Ufaransa dakika ya 56, kabla ya mkongwe wa Barcelona, Robert Lewandowski dakika ya 79.
Kwa matokeo hayo, Austria imeongza Kundi D kwa pointi zake sita ikifuatiwa na Ufaransa pointi tano na zote zinafuzu Hatua ya 16 Bora, wakati Uholanzi iliyomaliza na pointi zake nne nafasi ya tatu itaangalia uwezekano wa kusonga mbele kama mmoja wa washindi wa tatu bora wanne na Poland yenye pointi moja inarudi nyumbani.
Katika mechi za mwisho za Kundi C, England ilitoa sare ya bila kufungana na Slovenia Uwanja wa RheinEnergie Jijini Cologne kama ilivyokuwa kwa Denmark na Serbia Uwanja wa Allianz Arena Jijini Munich.
Kwa matokeo hayo, England imemaliza kileleni mwa kundi hilo kwa pointi zake tano ikifuatiwa na Denmark pointi tatu na zote zinakwenda Hatua ya 16 Bora, wakati Slovenia iliyomaliza na pointi tatu pia itakwenda kujaribu kupenya kupitia kapu la washindi wa tatu bora wanne na Serbia yenye pointi mbili inarejea nyumbani.
0 comments:
Post a Comment