KATIBU Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Gerson Msigwa amesema kuwa kuelekea mashindano ya AFCON 2027, Tanzania iko katika maandalizi ya Mkakati maalum utakaotekelezwa ili kufanikisha mashindano hayo makubwa Barani Afrika pamoja na kuainisha majukumu mbalimbali yatakayotekelezwa na Serikali na wadau wa Sekta Binafsi ili Tanzania inufaike kikamilifu na fursa zitakazotokana uenyeji wa mashindano hayo.
Akizungumza juzi (Aprili 16, 2024) Jijini Dar Es Salaam mara baada ya kukutana na Kamati maalum ya kuandaa Mkakati ya AFCON 2027 ambayo pia imewasilisha andiko la kwanza la mkakati huo, Katibu Mkuu Msigwa amesema kamati hiyo inaandaa mchoro wa jinsi gani michuano ya mataifa ya Afrika AFCON 2027 itakayofanyika nchini Tanzania, Kenya na Uganda itawanufaisha Watanzania katika nyanja mbalimbali nje ya soka.
‘Wizara tumeona ni muhimu tuwe na muongozo ambao utatuonesha ni vitu gani tufanye sasa, kabla, wakati wa mashindano na baada ya mashindano ambayo ni muhimu kuyajua kwa sababu mashindano haya yanakuja na vitu vingi tofauti na soka ikiwemo biashara,utalii na uwekezaji’ Amesisitiza Msigwa
Aidha, ametoa wito kwa Watanzania waanze maandalizi ya kuchangamkia fursa zitakazoletwa na michuano hiyo ili wanufaike kiuchumi.
0 comments:
Post a Comment