KIUNGO Mganda wa Yanga, Khalid Aucho leo amefanya mazoezi kikamilifu kuelekea mchezo wa kwanza wa Robó Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mamelodi Sundowns Jumamosi Uwanja wa Benjamín Mkapa Jijini Dar es Salaam.
Aucho aliumia kwenye mchezo wa mwisho wa Kundi D Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly Machi 1 mwaka huu Uwanja wa Cairo International Jijini Cairo nchini Misri.
Katika mchezo huo, Aucho alishindwa kuendelea dakika ya 73, nafasi yake ikichukuliwa na Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Yanga ikichapwa 1-0 bao pekee la Hussein El Shahat dakika ya 46.
Wachezaji wengine waliokuwa wanasumbuliwa na maumivu, beki Kibwana Shomari, kiungo Zawadi Mauya wote wamefanya mazoezi vizuri leo - na shaka bado ipo kwa nyota wa Ivory Coast, beki Kouassi Attohoula Yao na kiungo Peodoh Pacôme Zouzoua.
Yanga watakuwa wenyeji wa Mamelodi Sundowns Jumamosi ya kuanzia Saa 3:00 usiku Uwanja wa Benjamín Mkapa Jijini Dar es Salaam, kabla ya timu hizo kurudiana Ijumaa ya Aprili 5 Uwanja wa Loftus Jijini Pretoria.
Mara ya mwisho timu hizo zilikutana katika Hatua ya 16 Bora Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2001 na Mamelodi Sundowns wakaitoa Yanga kwa jumla ya mabao 6-5, wakishinda 3-2 Pretoria na kutoa sare ya 3-3 Uwanja wa CCM Kirumba Jijini Mwanza.
Mshindi wa jumla baina ya Yanga na Mamelodi Sundwons atakutana na mshindi wa jumla katí ya Esperance ya Tunisia na ASEC Mimosas ya Ivory Coast.
0 comments:
Post a Comment