RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia leo amekabidhiwa jezi za Simba na Yanga kuelekea mechi za kwanza za Robó Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika wikiendi ijayo Jijini Dar es Salaam.
Hii ni katika kuunga mkono agizo la Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Damas Ndumbaro kwamba mashabiki wa timu hizo waungane kusapoti timu hizo za nyumbani dhidi ya wageni Al Ahly ya Misri na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.
Simba SC watakuwa wenyeji wa Al Ahly katika mchezo wa kwanza wa Robó Fainali Ijumaa ya Machi 29 kuanzia Saa 3:00 usiku Uwanja wa Benjamín Mkapa Jijini Dar es Salaam, kabla ya timu hizo kurudiana Ijumaa itakayofuata Aprili 5 Uwanja wa Cairo International Jijini Cairo, Misri.
Ikumbukwe mwishoni mwa mwaka jana timu hizo zilikutana katika Robó Fainali ya michuano mipya, African Football League na kutoa sare ya jumla ya 3-3, wakifungana 2-2 Oktoba 20 Dar es Salaam na 1-1 Oktoba 24 Cairo, hivyo Al Ahly kwenda Nusu Fainali kwa faida ya mabao ya ugenini.
Mshindi wa jumla katí ya Simba na Al Ahly atakutana na mshindi wa jumla katí ya TP Mazembe na Petro de Luanda ya Angola katika Nusu Fainali.
Kwa upande wao Yanga watakuwa wenyeji wa Mamelodi Sundowns Jumamosi ya Machi 30 kuanzia Saa 3:00 usiku Uwanja wa Benjamín Mkapa Jijini Dar es Salaam, kabla ya timu hizo kurudiana Ijumaa ya Aprili 5 Uwanja wa Loftus Jijini Pretoria.
Mara ya mwisho timu hizo zilikutana katika Hatua ya 16 Bora Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2001 na Mamelodi Sundowns wakaitoa Yanga kwa jumla ya mabao 6-5, wakishinda 3-2 Pretoria na kutoa sare ya 3-3 Uwanja wa CCM Kirumba Jijini Mwanza.
Mshindi wa jumla baina ya Yanga na Mamelodi Sundwons atakutana na mshindi wa jumla katí ya Esperance ya Tunisia na ASEC Mimosas ya Ivory Coast.
0 comments:
Post a Comment