WENYEJI, Arsenal wamefanikiwa kwenda hatua ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya ushindi wa penalti 4-2 kufuatia ushindi wa 1-0 usiku wa Jumanne Uwanja wa Emirates Jijini London.
Kwa ushindi huo timu zinakuwa zimefungana kwa sare ya jumla 1-1 kufuatia FC Porto kushinda 1-0 mechi ya kwanza Februari 21 nchini Ureno.
Bao pekee la Arsenal usiku wa jana lilifungwa na mshambuliaji Mbelgiji, Leandro Trossard dakika ya 41.
Na kwenye mikwaju ya penalti waliofunga upande wa Arsenal ni Martin Ødegaard, Kai Lukas Havertz, Bukayo Saka na Declan Rice.
Upande wa Porto waliofunga ni Pepê Aquino na Marko Grujić pekee huku Wendell Borges na Wenderson Galeno penalti zao ziliokolewa na kipa David Raya.
Mechi nyingine ya marudiano 16 Bora Ligi ya Mabingwa Ulaya, Barcelona iliichapa Napoli 3-1 Uwanja wa Venue Estadi Olímpic Lluís Companys mjini Barcelona.
Mabao ya Barcelona yalifungwa na Fermín dakika ya 15, João Cancelo dakika ya 17 na Robert Lewandowski dakika ya 83, huku bao pekee la Napoli likifungwa na Amir Rrahmani dakika ya 30.
Kwa matokeo hayo Barca wanakwenda Robó Fainali kwa ushindi wa 4-2 kufuatia sare ya 1-1 kwenye mchezo wa kwanza Italia.
Timu nyingine zilizofuzu Robó Fainali ni mabingwa watetezi, Manchester City, Real Madrid, Paris Saint-Germain na Bayern Munich.
Timu nyingine mbili zitapatikana baada ya mechi mbili za mwisho leo; Atletico Madrid na Inter Milan nchini Hispania na Borussia Dortmund dhidi ya PSV Eindhoven nchini Ujerumani.
Mechi za kwanza Inter Milan iliichapa Atletico Madrid 1-0 Italia na PSV ikatoa sare ya 1-1 na Borussia Dortmund.
0 comments:
Post a Comment