WENYEJI, Yanga SC wameibuka na ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya CR Belouizdad ya Algeria katika mchezo wa Kundi D Ligi ya Mabingwa Afrika usiku huu Uwanja wa Benjamín Mkapa Jijini Dar es Salaam.
Mabao ya Yanga yamefungwa na viungo, mzawa Mudathir Yahya Abbas ‘Zanzíbar Greatest’ dakika ya 43 na Mburkinabe, Stephane Aziz Ki dakika ya 47 na washambuliaji, Mzambia Kennedy Musonda dakika ya 48 na Muivory Coast, Joseph Guede Gnadou dakika ya 84.
Kwa ushindi huo, Yanga SC inayofundishwa na Kocha Muargentina, Miguel Ángel Gamondi inafikisha pointi nane na kusogea nafasi ya pili, nyuma ya mabingwa watetezi, Al Ahly ya Misri baada ya wote kucheza mechi tano.
Kwa upande wao CR Belouizdad wanabaki na pointi zao tano, mbele ya Medeama SC ya Ghana yenye pointi nne inayoshika mkia baada ya wote kucheza mechi tano pia.
Matokeo haya yanamaanisha Yanga imejihakikishia tiketi ya Robo Fainali kabla ya mechi za mwisho Machi 1 hata CR Belouizdad wakishinda dhidi ya Medeama SC kwa idadi ya kubwa mabao.
Kanuni za Shirikisho la Soka Afrika (CAF) zinasema timu zikilingana kwa pointi mshindi ataamuliwa kwa motokeo ya jumla baina yao na inakumbukwa CR Belouizdad ilishinda 3-0 dhidi ya Yanga kwenye mchezo wa kwanza Novemba 24 mwaka jana Jijini Algiers.
Machi 1 Yanga watakuwa wageni wa Al Ahly Uwanja wa Cairo International, Cairo nchini Misri na CR Belouizdad watakuwa wenyeji wa Medeama Uwanja wa Julai 5, 1962 Jijini Algiers nchini Algeria zote zikianza Saa 1:00 usiku.
0 comments:
Post a Comment