MABINGWA watetezi, Senegal jana wamefanikiwa kwenda Hatua ya Mtoano ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika baada ya ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Cameroon katika mchezo wa Kundi C Uwanja Charles Konan Banny mjini Yamoussoukro, Ivory Coast.
Mabao ya Simba wa Teranga yalifungwa na washambuliaji Ismaïla Sarr wa Marseille ya Ufaransa dakika ya 16, na nyota wanaocheza Saudi Arabia, Mouhamadou Habibou Diallo wa Al Shabab dakika ya 71 na Nahodha Sadio Mané wa Al Nassr dakika ya 90 na ushei, wakati bao pekee la Simba wa Teranga lilifungwa na wa Jean-Charles Victor Castelletto Nantes ya Ufaransa dakika ya 83.
Mechi nyingine ya Kundi C, Guinea iliichapa Gambia 1-0, bao pekee la kiungo wa Atromitos ya Ugiriki, Aguibou Camara dakika ya 69 hapo hapo Uwanja Charles Konan Banny.
Senegal ipo kileleni mwa Kund C kwa pointi zake sita, ikifuatiwa na Guinea yenye pointi nne, Cameroon pointi moja na Gambia ambayo haina pointi inashika mkia.
Sasa Cameroon italazimika kuifunga Gambia mabao ya kutosha na kuomba Senegal iifunge Guinea ili kufuzu Hatua ya Mtoano angalau kwa wastani wa mabao.
Mechi pekee ya Kundi B jana, Cape Verde walikata tiketi ya kwenda Hatua ya Mtoano baada ya ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Msumbiji, mabao ya mshambuliaji wa Rayo Vallecano ya Hispania, Tiago Manuel Dias Correia ‘Bebé’ dakika ya 32, winga wa Fatih Karagümrük ya Uturuki, Ryan Mendes dakika ya 51 na kiungo wa Krasnodar ya Urusi,Kevin Pina dakika ya 69 Uwanja wa Félix Houphouët-Boigny Jijini Abidjan.
Cape Verde inaongoza Kundi B kwa pointi zake sita, ikifuatiwa na Misri pointi mbili, Ghana na Msumbiji moja kila moja kuelekea mechi za mwisho. Misri itamaliza na Cape Verde na Ghana itamaliza na Msumbiji.
0 comments:
Post a Comment