TIMU ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) imefanikiwa kwenda Robó Fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika baada ya ushindi wa penalti 8-7 dhidi ya Misri kufuatia sare ya 1-1 ndani ya dakika 120 usiku wa kuamkia leo Uwanja wa Laurent Pokou mjini San-Pedro nchini Ivory Coast.
DRC walitangulia kwa bao la mshambuliaji wa Young Boys ya Uswisi Meschack Elia Lina dakika ya 37, kabla ya mshambuliaji wa Nantes ya Ufaransa, Mostafa Mohamed kuisawazishia Misri kwa penalti dakika ya 45.
Pamoja na Misri kumaliza pungufu kufuatia mchezaji wake Hamdi Mohamed kutolewa kwa nyekundu katika dakika za nyongeza kufuatia kuonyeshwa kadi ya pili ya njano, lakini ilifanikiwa kumaliza dakika 120 na kwenda kwenye mikwaju ya penalti.
Waliofunga penalti za DRC ni Samuel Moutoussamy (Nantes, Ufaransa), Grady Diangana (West Bromwich Albion, England), Silas Katompa (Stuttgart, Ujerumani), Aaron Tshibola (Hatta, Dubai), Gédéon Kalulu (Lorient, Ufaransa), Chancel Mbemba (Marseille, Ufaransa), Henock Inonga (Simba SC, Tanzania) na kipa Lionel Mpasi-Nzau (Rodez, Ufaransa), wakati Arthur Masuaku wa Besiktas ya Uturuki pekee alikosa.
Waliofunga penalti za Misri ni Mohamed Abdelmonem (Al Ahly), Omar Marmoush ( Eintracht Franfurt, Ujerumani), Omar Kamal (Al Ahly), Mohamed Hany (Al Ahly), Ahmed Hegazy ( Al Ittihad, Saudi Arabia), Mostafa Fathi (Pyramids) na Mahmoud Hamada (Al Masry), wakati Mostafa Mohamed (Nantes, Ufaransa) na kipa Mohamed Abou Gabal 'Gabaski' wa Al Ahly walikosa.
Sasa DRC itakutana na Guinea ambayo mapema jana iliitoa Equatorial Guinea kwa kuichapa 1-0, bao pekee la mshambuliaji wa Le Havre ya Ufaransa, Mohamed Lamine Bayo dakika ya 90 Olympique Alassane Ouattara Jijini Abidjan.
Equatorial Guinea ilimpoteza Féderico Bikoro aliyetolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 55, kabla ya Nahodha wake na kinara wa mabao AFCON ya mwaka huu hadi sasa, Emilio Nsue wa Intercity ya Hispania kukosa penalti dakika ya 69.
0 comments:
Post a Comment