TIMU ya Afrika Kusini imefanikiwa kutinga Robo Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika baada ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Morocco usiku wa kuamkia leo Uwanja wa Laurent Pokou mjini San-Pedro nchini Ivory Coast.
Mabao ya Bafana Bafana yalifungwa na Evidence Makgopa dakika ya 57 na Teboho Mokoena dakika ya 90 na ushei.
Haikuwa siku kabisa kwa Simba wa Atlasi, kwani mbali na Achraf Hakimi kugongesha kwenye nguzo mkwaju wa penalti dakika ya 83 uliotolewa na Refa Mahmood Ismail wa Sudan baada ya Teboho Mokoena kuunawa mpira, lakini Sofyan Amrabat alitolewa kwa kadi nyekundu baada ya kumchezea rafu Mokoena dakika ya 90 na ushei.
Bafana Bafana itakutana na Cape Verde Jumamosi ya Februari 3 Uwanja wa Charles Konan Banny mjini Yamoussoukro katika Robo Fainali.
Katika mchezo uliotangulia wa Hatua ya 16 Bora jana, Mali iliitupa nje Burkina kwa kuichapa mabao 2-1 Uwanja wa Amadou Gon Coulibaly mjini Korhogo.
Mabao ya Mali yalifungwa na Edmond Tabsoba aliyejifunga dakika ya tatu na Lassine Sinayoko dakika ya 47, huku la Burkina Faso likifungwa na Nahodha wake, Bertrand Traore dakika ya 57.
Mali itakutana na wenyeji, Ivory Coast katika Robo Fanali Jumamosi.
Robo Fainali nyingine ni Nigeria na Angola na DRC dhidi ya Guinea Ijumaa ya Februari 2.
0 comments:
Post a Comment