TIMU ya Simba SC imepoteza mechi ya kwanza ya Kundi B Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuchapwa 1-0 na wenyeji, Wydad Club Athletic usiku huu Uwanja wa Marrakech Jijini Marrakech nchini Morocco.
Simba ilikaribia kabisa kumaliza mechi zake tatu za mwanzo za Kundi B kwa sare tupu baada ya sare ya 1-1 nyumbani na ASEC Mimosas na 0-0 na Jwaneng Galaxy ugenini, lakini bao la kiungo Mualgeria Zakaria Draoui dakika ya 90 na ushei likaharibu utaratibu.
Lakini sifa kwake kipa Ayoub Lakred aliyeokoa penalti ya Mmorocco mwenzake, Yahya Jabrane dakika ya 40.
Mechi nyingine ya Kundi B mapema jana ASEC Mimosas iliwachapa wenyeji, Jwaneng Galaxy 2-0 Jijini Francistown nchini Botswana na sasa timu hiyo ya Ivory Coast inafikisha pointi saba kileleni.
Jwaneng Galaxy yenye pointi nne sasa ni ya pili, Wydad Athletic yenye pointi tatu ni ya tatu na Simba inashika mkia kwa pointi zake mbili.
Mechi zijazo, Simba SC watakuwa wenyeji wa Wydad Jumanne ya Desemba 19 Saa 10:00 jioni Dar es Salaam na ASEC Mimosas watakuwa wenyeji wa Jwaneng Galaxy Saa 1:00 usiku Jijini Abidjan.
0 comments:
Post a Comment