TIMU ya JKT Queens jana imeweka hai matumaini ya kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Afrika kwa Wanawake baada ya ushindi wa 2-1 dhidi ya wenyeji, Athlético Abidjan katika mchezo wa KundinA Uwanja wa Amadou Gon Coulibaly mjini Korhogo nchini Ivory Coast.
Mabao ya JKT Queens jana yalifungwa na viungo na mabinti wadogo, Winfrida Hubert Gerald (15) dakika ya 66 na Aaliyah Fikiri Salum (17) dakika ya 85, baada ya Athlético Abidjan kutangulia na bao la Adjoua Edwige Sandrine Niamien (29) dakika ya 33.
Kwa matokeo hayo, JKT Queens inaokota pointi tatu za kwanza kundini, ikitoka kupoteza mechi yake ya kwanza kwa kuchapwa 2-0 na Mamelodi Sundowns kwenye mchezo wa kwanza, wakati Athlético Abidjan inabaki na pointi yake moja iliyovuna kwenye sare ya 1-1 na Sporting Casablanca ya Morocco kwenye mechi ya ufunguzi.
Mamelodi Sundowns ambayo jana iliilaza Sporting Casablanca 1-0 ndio inaongoza Kundi A kwa ponti zake sita na imekwishajikatia tiketi ya Nusu Fainali.
Mechi za mwisho za Kundi A zitachezwa muda mmoja, Saa 5:00 usiku Mamelodi Sundowns na Athlético Abidjan Uwanja wa Amadou Gon Coulibaly mjini Korhogo na JKT Queens dhidi ya Sporting Casablanca Uwanja wa Laurent Pokou mjini San-Pedro.
0 comments:
Post a Comment