MSHAMBULIAJI Mkongo, Jean Othos Baleke amefunga mabao yote Simba ikiibuka na ushindi wa 3-0 dhidi ya Coastal Unión ya Tanga katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara leo Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam.
Baleke ambaye yupo katika msimu wake wa pili Simba baada ya kusajiliwa dirisha dogo, Januari mwaka huu akitokea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), amefunga mabao hayo dakika za saba, 11 na 40 kwa penalti baada ya kiungo wa Kimataifa wa Msumbiji, Luis Jose Miquissone kuchezewa rafu kwenye boksi.
Coastal Union ilimaliza pungufu baada ya mshambuliaji wake, Haji Ugando kutolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 19 kufuatia kumchezea rafu beki wa Simba, Mkongo Henock Inonga Baka ‘Varane’ aliyeshindwa kuendelea na mchezo nafasi yake ikichukuliwa na Kennedy Juma dakika ya 24.
Simba SC inafikisha pointi tisa na kuungana na watani wao, Yanga ambao wanaendelea kuongoza Ligi kwa wastani wa mabao, wakati Coastal Unión inabaki na pointi moja baada ya wote kucheza mechi tatu.
0 comments:
Post a Comment