WIZARA ya Utamaduni, Sanaa na Michezo imesaini Mkataba wa makubaliano ya ukarabati wa Uwanja wa Benjamin Mkapa na Kampuni ya Beijing Construction Engineering Group (BCEG) ya China ambao utagharimu zaidi ya Sh. Bilioni 31 hadi kukamilika Julai 2024.
Hayo yamesemwa Dar es Salaam Julai 27, 2023 na Waziri wa Wizara hiyo, Mhe. Dkt. Pindi Chana baada ya kushuhudia Utiaji saini wa mkataba huo na kampuni BCEG ya China ambao pia ndio waliojenga uwanja huo.
Alisema lengo la ukarabati huo ni kufikia viwango vya Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) Pamoja na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) ili uendelee kuwa bora zaidi.
"Wito wangu kwa kampuni ya BCEG, hakikisheni kazi hii mnayoifanya iwe ya viwango vinavyowekwa iendane na ubora na viwango vya CAF na FIFA na ikamilike kwa wakati” amesema Dkt. Chana.
Naye Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Bw. Said Yakubu amesema uwanja huo utafanyiwa marekebisho katika eneo la vyumba vya wachezaji, chumba cha waandishi wa Habari, eneo la watu mashuhuri (VVIP), kubadilisha viti vyote vya kukalia mashabiki uwanjani hapo, ubao wa kuonesha matokeo, kuweka mfumo mpya wa TEHAMA, kubadilisha eneo la kuchezea na seti mbili za magoli ambazo zitatumika uwanjani hapo.
Maeneo mengine ambayo yatafanyiwa ukarabati ni viti vya benchi la ufundi na wachezaji wa akiba, mfumo wa umeme, mfumo wa sauti, eneo la kukimbilia wanariadha, chumba cha VAR, lifti mbili mpya, mfumo wa taa, mfumo wa maji taka, mgahawa pamoja na vitu vingine ambavyo vimepita muda wa matumizi kwani vilitakiwa kutumika kwa muda wa miaka saba tu.
Aidha, Katibu Mkuu Yakubu ametoa wito kwa watumiaji wa uwanja huo wakiwemo mashabiki, kuhakikisha wanatunza miundombinu ya uwanja huo ili iendelee kutumika kadiri ilivyopangwa na kuendelea kuwa eneo la watanzania kupata burudani wakati wa kuangalia mechi mbalimbali na nchi jirani wanaoutumia kama uwanja wao wa nyumbani.
Katika kufanikisha ukarabati huo, Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) watatoa viti vipya vitakavyotumiwa na benchi la ufundi pamoja na wachezaji wa akiba.
0 comments:
Post a Comment