CHAMA cha Waandishi wa Michezo Tanzania (TASWA) na Taasisi ya Uhusiano wa Umma Tanzania (IPRT), wamesaini makubaliano ya ushirikiano wa kimkakati wenye lengo la kukuza na kuendeleza waandishi wa habari za michezo na tasnia ya michezo kwa ujumla.
Tukio la kusaini Mkataba wa Ushirikiano(MoU) limefanyika leo jijini Dar es Salaam, likihusisha viongozi waandamizi wa taasisi hizo mbili akiwemo Mwenyekiti wa TASWA Amir Mhando, Katibu Mkuu wa chama hicho Alfred Lucas na Mkurugenzi wa IPRT William Kallaghe.
Akizungumza baada ya kusaini makubaliano hayo Kallaghe amesema wamehitimisha mazungumzo ya muda mrefu na uongozi wa chama hicho kuona namna ya kuwepo mafunzo ya kitaaluma na ya sekta ya michezo kwa waandishi wa habari za michezo na wachambuzi wa habari za michezo kwa ujumla.
“Kutakuwa na programu ya mafunzo maalum ya mawasiliano na uongozi, ambayo imeandaliwa kwa ajili ya watendaji wakuu na itajikita katika kuendeleza ufahamu sahihi wa maadili na ujuzi wa ngazi ya chini na juu ili kufikia malengo ya mafanikio kitaasisi.
“Pia kutakuwa na mafunzo ya wazi ya mawasiliano na uongozi, eneo hili ni maalum kwa ajili ya wahariri wa habari za michezo, wasemaji wa klabu na vyama vya michezo.
“Eneo lingine ni mafunzo kwa waandishi wa habari za michezo na wachambuzi, hii ni programu ya maalum inayolenga kuwajengea uwezo waandishi wa habari za michezo, waandishi waandamizi wa habari za michezo na wachambuzi wa habari za michezo,” amesema Kallaghe.
Kwa upande wake Mhando amesema eneo lingine ambalo limetiliwa mkazo ni mafunzo ya uwezeshaji wa wanawake waandishi wa habari za michezo ili kuwajengea uwezo zaidi.
0 comments:
Post a Comment