TIMU za Simba na Yanga zimekamilisha mechi zao za makundi bila ushindi katika Ligi ya Vijana chini ya umri wa miaka 20, michuano inayoendelea Uwanja wa Azam Complex, Chamazi Jijini Dar es Salaam.
Yanga imetoa sare ya 1-1 na Polisi Tanzania katika mchezo wa Kundi B bao la wana Jangwani likifungwa na Fred Dennis huku la Maafande likifungwa na Jackson Hizza.
Nayo Simba imechapwa 2-0 na Azam FC mabao ya Daudi Said na Cyprian Kachwele katika mchezo wa Kundi D, huku mechi za leo Dodoma Jiji wakishinda 4-2 dhidi ya Tanzania Prisons Kundi B na Kagera Sugar wakiichapa Ihefu SC 4-0 Kundi D.
Azam FC iliyokusanya pointi zote tisa imekwenda Robo Fainali pamoja na Kagera Sugar iliyomaliza na pointi nne Kundi D, huku Dodoma Jiji ikiongoza Kundi B kwa pointi zake saba mbele ya Tanzania Prisons pointi sita na zote zimekwenda Robo Fainali.
Timu nyingine zilizokwenda Robó Fainali ni mabingwa watetezi, Mtibwa Sugar na Mbeya City kutoka Kundi A na Geita Gold na Coastal Unión kutoka Kundi C.
Robo Fainali zote zitachezwa Jumatano hapo hapo Chamazi; Mtibwa Sugar na Coastal Union, Dodoma Jiji na Kagera Sugar, Geita Gold na Mbeya City na Azam FC dhidi ya Tanzania Prisons.
0 comments:
Post a Comment