RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samiah Suluhu Hassan amewapa ndege Yanga iwapeleke Mbeya kumalizia mechi zao za Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara.
Uongozi wa Yanga umesema walipanga kuondoka leo jioni kwenda Mbeya kwa ajili ya mechi zao mbili za mwisho, lakini kutoka na mwaliko wa Rais Samia Ikulu kwa chakula cha jioni hawataweza kuiwahi tena ndege hiyo.
Ni kwa sababu hiyo, Rais Samia ametoa ndege maalum ambayo itaondoka Saa 5:00 usiku wa leo kwenda Mbeya kwa ajili ya mchezo wao wa kesho dhidi ya Mbeya City Uwanja wa Sokoine.
Rais Dk. Samiah Suluhu Hassan ambaye aliwapa Yanga ndege ya kwenda Algeria na kurudi, amewaalika kwa chakula cha jioni leo Ikulu Jijini Dar es Salaam ikiwa ni pongezi zake kwao kwa kushika nafasi ya pili kwenye Kombe la Shirikisho Afrika.
Yanga juzi ilipata ushindi wa 1-0 dhidi ya USM Alger katika mchezo wa marudiano wa Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika Uwanja wa Julai 5, 1962 Jijini Algiers nchini Algeria.
Lakini ni USM Alger waliofanikiwa kutwaa Kombe hilo kwa faida ya mabao ya ugenini kufuatia ushindi wa 2-1 kwenye mchezo wa kwanza Jumapili iliyopita Jijini Dar es Salaam.
USM Alger wamenufaika na ushindi wa ugenini wa 2-1 kwenye mchezo wa kwanza, kwani pamoja na sare ya jumla ya 2-2, lakini wamefaidika na mabao ya ugenini.
Katika mchezo wa juzi bao pekee la Yanga lilifungwa na beki wa kulia, Juma Shabani kwa penalti dakika ya saba baada ya Mzambia Kennedy Musonda kuangushwa kwenye boksi.
Kipa wa Kimataifa wa Mali, Djigui Diarra aliinusuru Yanga kuruhusu bao leo baada ya kupangua mkwaju wa penalti wa beki Zinéddine Belaïd dakika ya 59 na baada ya mchezo akapewa Tuzo ya Mchezaji Bora wa Mechi.
Mshambuliaji Fiston Kalala Mayele ameibuka Mfungaji Bora wa Kombe la Shirikisho kwa mabao yake saba.
0 comments:
Post a Comment