VIGOGO, Simba SC wameisindikiza Polisi Tanzania kushuka daraja kwa kuitandika mabao 6-1 katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara leo Uwanja wa Azam Complex, Chamazi Jijini Dar es Salaam.
Nyota wa mchezo wa leo alikuwa ni kiungo mshambuliaji Mrundi, Saido Ntibanzokiza aliyefunga mabao matano peke yake dakika za 16, 21,27 , 79 na 89, huku lingine likifungwa na Israel Mwenda dakika ya 66.
Bao la kufuatia machozi la Polisi Tanzania limefungwa na mshambuliaji kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Henock Mayala dakika ya 85.
Simba SC inafikisha pointi 70 na kuendelea kushika nafasi ya pili nyuma ya Mabingwa tayari kwa mara ya pili ya mfululizo, Yanga wenye pointi 75 baada ya wote kucheza mechi 29.
Polisi Tanzania inabaki na pointi zao 25 na rasmi inaungana na Ruvu Shooting yenye pointi 20 baada ya wote kucheza mechi 29 pía kuipa mkono wa kwaheri Ligi Kuu.
Kwa Ntibanzokiza sasa amefikisha mabao 15 na kupanda hadi nafasi ya pili kwenye chati ya ufungaji akizidiwa moja tu na mshambuliaji Mkongo wa Yanga, Fiston Kalala Mayele anayeongoza kuelekea mechi za mwisho Ijumaa.
0 comments:
Post a Comment