KLABU ya Yanga imetangaza kuchana na beki wake wa katí, Abdallah Haji Shaibu ‘Ninja’, huyo akiwa mchezaji wa tano kuondoka baada ya msimu mzuri wa mafanikio.
“Tunamshukuru Abdallah Shaibu (Ninja) kwa mchango wake katika kipindi chote alichokuwa nasi na tunamtakia kila la kheri katika maisha yake mapya nje ya Young Africans SC,” imesema taarifa Yanga jioni hii.
Ninja alijiunga na Yanga kwa mara ya kwanza mwaka 2017 akitokea ya kwao, Zanzíbar kabla ya kuuzwa MFK Vyškov ya Jamhuri ya Czech, mwaka 2019 ambayo ilimpeleka kwa mkopo LA Galaxy II ya Marekani alikocheza hadi mwaka 2020 akarejea Jangwani.
Msimu uliopita Ninja alipelekwa kwa mkopo Dodoma Jiji, kabla ya kurejeshwa dirisha dogo lakini hakuweza kumshawishi Kocha Mtunisia, Nasredeen Nabi.
Abdallah Shaibu ‘Ninja’ anakuwa mchezaji wa tano kuondoka Yanga baada ya kiungo Mzanzibari Feisal Salum aliyeuzwa Azam FC, mawinga Mghana, Bernard Morrison, Mkongo Tuisila Kisinda na mzawa, Dickson Ambundo.
Tayari Yanga imeachana na Kocha wake Mkuu, Mtunisia Nasredeen Nabi na Kocha wa makipa, Mbrazil Milton Nienov.
0 comments:
Post a Comment