TIMU ya Yanga SC ya Tanzania imefanikiwa kwenda Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya wenyeji, Marumo Gallants usiku huu Uwanja wa Royal Bafokeng, Phokeng NW Jijini Rustenburg nchini Afrika Kusini.
Ilikuwa siku nzuri ofisini kwa mshambuliaji wa Kimataifa wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Fiston Kalala Mayele aliyefunga bao la Kwanza dakika ya 45, kabla ya kumsetia Mzambia, Kennedy Musonda kufunga la pili dakika ya 62.
Marumo Gallants walipata bao lao pekee kupitia kwa mshambuliaji wao, Ranga Piniel Chivaviro dakika ya 90 na ushei, hivyo kuendelea kufungana na Mayele kwneye chati ya ufungaji kila mmoja akiwa na mabao saba.
Yanga wanakwenda Fainali kwa ushindi wa jumla wa 4-1 kufuatia kuwafunga Marumo Gallants 2-0 kwenye mchezo wa Kwanza Jumatano iliyopita Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.
Yanga itaanzia nyumbani katika Fainali ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya USM Alger Mei 28 Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam kabla ya kwenda Algeria kwa mchezo wa marudiano Juni 3 Uwanja wa Julai 5, 1962 Jijini Algiers.
USM Alger imeitoa ASEC Mimosas ya Ivory Coast baada ya sare ya 0-0 ugenini na ushindi wa 2-0 nyumbani.
0 comments:
Post a Comment