WIZARA ya Utamaduni, Sanaa na Michezo imesaidia kugharamia usafiri wa mashabiki 55 wa timu ya Yanga kwenda Afrika Kusini katika mchezo wa pili wa hatua ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAF) huku Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Hamis Mwinjuma akitarajia kuongoza msafara huo.
Hayo yamebainishwa na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Saidi Yakubu ikiwa ni hatua ya kuiunga mkono timu ya Yanga ambao wanatarajia kucheza mchezo wa pili wa hatua ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya timu ya Marumo Gallants katika mchezo uliopangwa kuchezwa Mei 17 2023 kwenye Uwanja wa Royal Bafokeng uliopo mji wa Rustenburg nchini humo.
Yakubu amesema kuwa Serikali imesaidia safari hiyo kwa kupeleka baadhi ya mashabiki 55 ambao wataondoka Jumapili Mei 14, 2023 na wataungana na Watanzania wanaoishi nchini Afrika Kusini ili kuwapa hamasa ya kutosha wachezaji kushinda mchezo huo muhimi kulelekea hatua ya fainali ya mashindano hayo.
"Hii safari Serikali imesaidia Yanga kupeleka baadhi ya mashabiki 55 ambao wataondoka kesho Jumapili kueleka Afrika Kusini na huko wataungana na Watanzania waishio Afrika Kusini katika kuhakikisha wanatoa sapoti ya kutosha, nimeongea na Balozi nawao wamejiandaa kuwapokea kwa sababu pia wameanda mabasi kutoka kila mji kuhakikisha Watanzania wanakuwa wengi”
Katibu Mkuu ameongeza kuwa "Katika mechi hizi, lolote linaweza kutokea lakini Serikali pamoja na Yanga kupitia idara tofauti tumejipanga vizuri, Waziri Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana anatoa salamu nyingi, pongezi na kuwatakia ushindi katika mchezo wa marudiano. Naibu Waziri Mhe. Hamisi Mwinjuma ataungana na nyinyi kwa upande wa Serikali na anapenda kukaa na mashabiki kushangilia muda wote," alisema Yakubu.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa timu ya Yanga, Andrew Ntime amesema kuwa wao kama timu wamejiandaa vizuri kuhakikisha wanapata matokeo kwenye mchezo huo huku akitoa shukrani kwa Serikali kuwa mstari wa mbele wakati wote wa mashindano hayo na kutoa mchango wake wa kupeleka mashabiki hao kwenye mchezo huo wa marudiano.
0 comments:
Post a Comment