MSAFARA wa Yanga SC ulioondoka Dar es Salaam jana kwenda Singida kwa ajili ya mechi mbili dhidi ya wenyeji, Singida Big Stars umelazimika kurejea Jijini baada ya ndege kushindwa kutua mkoani humo.
Uongozi umewatoa hofu wapenzi na wanachama wake kwamba wachezaji wake wote na wana msafara mzima kwa ujumla wapo salama na sasa wanafanya utaratibu wa kupata ndege nyingine ili warejee Singida.
Yanga inakabiliwa na ratiba ngumu mno ya kucheza mechi tatu za mashindano tofauti ndani ya siku saba katika miji miwili, Singida na Dar es Salaam.
Alhamisi itakuwa mechi ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara na Jumapili Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC) zote dhidi ya Singida Uwanja wa LITI.
Baada ya hapo watasafiri kurejea Dar es Salaam kwa mchezo wa kwanza wa Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Marumo Gallants ya Afrika Kusini Jumatano ijayo, Mei 10.
Kwa mujibu wa ratiba ya Ligi Kuu, Yanga imebakiza jumla mechi nne za Ligi Kuu pamoja na huo wa Singida Big Stars, nyingine dhidi ya Dodoma Jiji, Mbeya City na Tanzania Prisons zote ugenini na wanatakiwa kushinda mechi tatu ili kuwa mabingwa tena.
Mechi ya marudiano na Marumo Gallants itafanyika Afrika Kusini Mei 17.
0 comments:
Post a Comment