TIMU ya Yanga SC ya Tanzania imefanikiwa kwenda Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya ushindi wa mabao 2-1 jana dhidi ya wenyeji, Marumo Gallants Uwanja wa Royal Bafokeng, Phokeng NW Jijini Rustenburg nchini Afrika Kusini.
Ilikuwa siku nzuri ofisini kwa mshambuliaji wa Kimataifa wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Fiston Kalala Mayele aliyefunga bao la Kwanza dakika ya 45, kabla ya kumsetia Mzambia, Kennedy Musonda kufunga la pili dakika ya 62.
Marumo Gallants walipata bao lao pekee kupitia kwa mshambuliaji wao, Ranga Piniel Chivaviro dakika ya 90 na ushei, hivyo kuendelea kufungana na Mayele kwneye chati ya ufungaji kila mmoja akiwa na mabao saba.
Yanga wanakwenda Fainali kwa ushindi wa jumla wa 4-1 kufuatia kuwafunga Marumo Gallants 2-0 kwenye mchezo wa Kwanza Jumatano iliyopita Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.
Yanga itakutana na USM Alger iliyoichapa 2-0 ASEC Mimosas jana Uwanja wa Julai 5, 1962 Jijini Algiers baada ya sare ya 0-0 kwenye mechi ya kwanza Jumatano iliyopita Uwanja wa Bouaké Jijini Bouaké nchini Ivory Coast.
Kwa mara ya kwanza klabu ya Tanzania itacheza Fainali michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika tangu ianzishwe mwaka 2004 kufuatia kufutwa kwa iliyokuwa michuano Kombe la CAF Cup na Kombe la Washindi, yote ikiendeshwa na bodi ya soka barani, CAF.
Mafanikio makubwa ya Tanzania kwa iliyokuwa michuano ya Kombe la Washindi Afrika ni Hatua ya Robo Fainali ambayo walifika hao hao Yanga mwaka 1995, ambako baada ya kuzitoa Vaal Reef Professionals ya Afrika Kusini na Tamil Cadets Club ya Mauritius, ikaenda kutolewa na Blackpool ya Zimbabwe.
Katika Kombe la CAF mafaniko makubwa ya Tanzania ni kufika Fainali kwa Simba SC, ambayo ilizitoa Ferroviario ya Msumbiji, Manzini Wanderers ya Swaziland, USM El Harrach ya Algeria katika Robo Fainali na AS Aviacao ya Angola katika Nusu Fainali kabla ya kufungwa na Stella Adjame ya Ivory Coast katika Fainali.
Zaidi ya hapo katika mfumo wa zamani wa Ligi ya Mabingwa Afrika, ikijulikana kama Klabu Bingwa Afrika – Yanga ilifika Robo Fainali mara mbili 1969 na 1970 na Simba Nusu Fainali mara moja mwaka 1974.
Mwaka 1969 Yanga ilizitoa Fitaridandro ya Madagascar na St. Georges ya Ethiopia, kabla ya kutolewa na Asante Kotoko ya Ghana baada ya kupigiwa kura ya sarafu kufuatia sare ya jumla ya 2-2, yaani 1-1 nyumbani na ugenini.
Mwaka 1970 Yanga ilizitoa US Fonctionnaires ya Madagascar na Nakuru All Stars ya Kenya, kabla ya kutolewa na Asante Kotoko kwa kufungwa 2-0 katika mechi ya tatu Jijini Addis Ababa, Ethiopia kufuatia sare ya 1-1 Dar es Salaam na 0-0 Ghana – hiyo ilikuwa kabla ya kuwekwa kwa sheria ya mabao ya ugenini kuhesabiwa mara mbili timu zinapotoa sare ya jumla.
Kwa upande wao, Simba mwaka 1974 walizitoa Linare ya Lesotho, Zambia Army na Hearts Of Oak ya Ghana katika Robo Fainali, kabla ya kutolewa na Ghazl El Mahalla ya Misri kwa penalti 3-0 kufuatia sare ya jumla ya 1-1, kila timu ikishinda 1-0 kwake.
Idadi ya mechi zimeongezeka tangu kuanzishwa kwa mfumo wa hatua ya makundi, ambayo imeongezea ugumu wa michuano.
Simba ilicheza na timu tano tu hadi Fainali mwaka 1993, ambazo ni Ferroviario ya Msumbiji, Manzini Wanderers ya Swaziland, USM El Harrach ya Algeria, AS Aviacao ya Angola na Stella Adjame ya Ivory Coast katika Fainali katika mechi 10.
Lakini kwa Yanga itakuwa na jumla ya mechi 16 dhidi ya wapinzani nane kuanzia Ligi ya Mabingwa Afrika ilipotolewa na Al Hilal Omdurman ya Sudan kabla ya kwenda kuitoa Club Africain ya Tunisa katika mchujo wa kuwania kucheza Hatua ya makundi kombe la Shirikisho Afrika.
Baadaye katika mechi za Kundi D ilifungwa na Monastir ya Tunisia pekee 2-0 Jijini Tunis, kabla ya kuzifunga 3-1 TP Mazembe, sare ya 1-1 na Réal Bamako nchini Mali, 2-0 zote Réal Bamako na Monastir Jijini Dar es Salaam na kwenda kumalizia kwa ushindi wa 1-0 dhidi ya TP Mazembe Jijini Lubumbashi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Katika Robo Fainali iliitoa Rivers United ya Nigeria kwa kuichapa 2-0 kwao na sare ya 0-0 nyumbani kabla ya kwenda kuitupa nje Marumo Gallants jana katika Nusu Fainali kwa kuichapa 2-1 Afrika Kusini ikitoka kushinda 2-0 Dar es Salaam.
Sasa Yanga itajaribu kuwa timu ya kwanza daima ya Tanzania kuwahi kutwaa Kombe lolote la Afrika itakapomenyana na USM Alger katika mechi mbili ngumu Mei 28 Dar es Salaam na Juni 3 Algiers.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan ameitumia salamu za pongezi Yanga kwa kuingia Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
“Pongezi za dhati kwa Klabu ya Yanga kwa kutinga Fainali ya Kombe la Shirikisho (CAF Confederation Cup). Mmeandika historia na kuipa nchi yetu heshima kubwa sana. Nawatakia kila la kheri katika mchezo wenu wa Fainali,” amesema Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.
Hongera Yanga kwa mafanikio haya chini ya kocha mtaalamu kabisa Nasredine Mohamed Nabi raia wa Tunisia, na kama alivyosema Mheshimiwa Rais Dk. Samia, mmeiheshimisha nchi. Kila la heri katika michezo wa Fainali.
0 comments:
Post a Comment