TIMU ya Simba SC imekamilisha mechi zake za Kundi C Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kuchapwa 3-1 na wenyeji, Raja Club Athletic usiku huu Uwanja wa Mfalme Mohamed V Jijini Casablanca nchini Morocco.
Mabao ya Raja yamefungwa na mshambuliaji Mmorocco, Hamza Khabba dakika ya 44 akimalizia pasi ya kichwa ya Yousri Bouzok na ya 70 kwa penalti baada ya yeye mwenyewe kuchezewa rafu kwenye boksi na beki Mkenya wa Simba, Joash Onyango na Mohamed Boulacsout dakika ya 86 akimalizia pasi ya kiungo Mualgeria, Abdelraouf Benguit.
Bao pekee la Simba limefungwa na mshambuliaji wake iliyemsajili dirisha dogo, Jean Bakeke dakika ya 48 akimalizia pasi ya kiungo wa kimataifa wa Tanzania, Muzamil Yassin Selemba.
Kwa matokeo hayo, Raja Casablanca inafikisha pointi 16 kileleni mwa Kundi C, ikifuatiwa na Simba yenye pointi tisa na zote zimefuzu Robo Fainali zikiziacha Horoya yenye pointi saba na Vipers pointi mbili zikiishia hatua ya 16 Bora.
0 comments:
Post a Comment