VIGOGO, Al Ahly jana wamefanikiwa kwenda Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya ushindi wa 3-0 dhidi ya Al Hilal Omdurman ya Sudan katika mchezo wa mwisho wa Kundi B Uwanja wa Kimataifa wa Cairo, Misri.
Mabao ya Al Ahly yalifungwa na Mahmoud ‘Kahraba’ Soliman dakika ya 25 na Hussein El Shahat dakika ya 64 na 81 na kwa matokeo hayo wanamaliza nafasi ya pili wakiwa na pointi 10, sawa na Al Hilal, lakini timu ya Misri inabebwa na wastani wa mabao.
Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini imeongoza kundi hilo kwa pointi zake 14, wakati Cotonsport ya Cameroon imeshika mkia baada ya kufungwa mechi zote za Kundi hilo nyumbani na ugenini.
Timu nne zilizoongoza makundi ni mabingwa watetezi, Wydad Casablanca A, Mamelodi B, Raja Casablanca ya Morocco C na Esperance ya Tunisia D.
Zilizoshika nafasi ya pili ni JS Kabylie ya Algeria A, Al Ahly B, Simba SC ya Tanzania C na CR Belouizdad ya Algeria pia Kundi D.
Droo ya mechi zote za Robo Fainali, pamoja na Kombe la Shirikisho Afrika itachezeshwa Jumatano makao makuu ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Jijini Cairo nchini Misri.
0 comments:
Post a Comment