WENYEJI, Yanga SC wamejiweka kwenye nafasi nzuri ya kwenda Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Real Bamako ya Mali katika mchezo wa Kundi D leo Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.
Mabao ya Yanga SC leo yamefungwa na mshambuliaji, Fiston Kalala Mayele dakika ya nane na Jesus Moloko dakika ya 68, huku Mkongo mwenzao, Yanick Bangala akikosa penalti dakika ya 57.
Mechi ya Kundi D iliyotangulia leo mjini Tunis, wenyeji Monastir wameshindwa 1-0 dhidi ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Sasa Monastir inaendelea kuongoza Kundi D kwa pointi zake 10, ikifuatiwa na Yanga pointi saba, Mazembe pointi tatu na Real Bamako pointi mbili.
Mechi zijazo Machi 19 Yanga SC watakuwa wenyeji wa Monastir Jijini Dar es Salaam na Real watawakaribisha TP Mazembe Jijini Bamako.
0 comments:
Post a Comment