KIKOSI cha Yanga kitaondoka Dar es Salaam Machi 30 kwenda Lubumbashi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kwa ajili ya mchezo wa mwisho wa Kundi D Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya wenyeji, TP Mazembe Aprili 2 Uwanja wa TP Mazembe mjini humo.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo, Afisa Habari wa klabu ya Yanga, Ally Kamwe amesema kwamba timu itarejea mazoezini kesho kwa wachezaji ambao hawajakwenda kwenye timu za taifa na itaingia kambini Machi 27.
amesema kikosi kitaondoka na ndege ya shirika la Tanzania (ATCL), ingawa wachezaji wengine wa kigeni waliokwenda kwenye zao za taifa wataungana nao huko huko Lubumbashi.
"Tuna idadi kubwa ya wachezaji walioitwa kwenye timu zao za taifa, wachezaji ambao wapo watarudi rasmi mazoezini kesho tayari kwa maandalizi ya mchezo wetu ujao na wa mwisho kwenye hatua ya makundi dhidi ya TP Mazembe ugenini.
"Na kambi rasmi ya mazoezi itaaanza tarehe 27 mwezi huu kwa ajili ya maandalizi ya mwisho kuelekea mchezo huo utaochezwa tarehe 2 mwezi ujao nchini Congo,"amesema Kamwe.
Aidha, Kamwe amesema kutakuwa na basi maalum la kusafirisha wanachama, mashabiki na wapenzi kwa gharama ya Sh. 700,000 kwenda na kurudi Aprili 3.
"Tunajivunia kuwa na mashabiki bora kwenye Klabu na hili tumelidhibitisha kwenye michezo yetu mitatu ya Kimataifa tukiwa nyumbani na sasa Uongozi wa Klabu umeamua lazima usafiri na mashabiki wake kwenda nao Congo kwenye mchezo wetu wa mwisho kwenye hatua ya makundi," ameongeza Kamwe.
Tayari ya Yanga imekwishafuzu Robo Fainali baada ya kujikusanyia pointi 10 katika michezo mitano na inakwenda Lubumbashi labda kusaka ushindi ili kujihakikishia kumaliza kileleni mwa kundi mbele ya US Monastirienne yenye pointi 10 pia.
0 comments:
Post a Comment