MWANARIADHA Alphonse Felix Simbu ameshinda Tuzo mbili za Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Mwanariadha Bora wa Kiume na Mwanamichezo Bora wa Mwaka 2022.
Katika sherehe hizo zilizofanyika usiku wa jana ukumbi wa Mlimani City Jijini Dar es Salaam, mshambuliaji wa Yanga Princess, Clara Luvanga ameshinda tuzo mbili pia, Mwanamichezo Bora wa Kike na Mwanasoka Bora wa Kike.
Simbu ametwaa tuzo hiyo baada ya kushinda medali ya fedha kwa upande wa Tanzania katika mashindano ya Jumuiya ya Madola yaliyofanyika mjini Birmingham, England huku Luvanga aliweza kuingoza vyema timu ya taifa ya wanawake wa chini ya miaka 17, Serengeti Girls kufuzu mashindano ya kombe la dunia nchini India. Manula ameiongoza vyema Simba kufuzu hatua ya mtoano ya kombe la shirikisho.
Mbali ya ushindi wa jumla, Simbu pia alishinda tuzo ya mwanariadha bora wa mwaka 2022. Washindani hao ni Yusuph Changarawe, Kasisim Mbutike ambao ni mabondia wa ngumi za ridhaa na bondia nyota wa ngumi za kulipwa, Ibrahim Mgander maarufu kwa jina la Ibrahim Class.
Mgeni rasmi katika tuzo hizo zilizofanyika kwenye ukumbi wa Mlimani City, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Pindi Chana alimkabidhi Simbu tuzo hizo zilizoandaliwa na BMT chini ya uratibu wa kampuni ya Radian na kudhaminiwa na Azam Media Limited, taasisi ya kifedha ya Faidika na NBC.
Katika usiku wa tuzo hizo, Rais Samia pia alipewa tuzo ya heshima ya kuchangia na kutia hamasa kuwa katika maendeleo ya michezo. Tuzo hiyoalipokea Waziri Chana kwa niaba yake.
Waziri Chana alimpongeza Simbu na wanamichezo wote walioshiriki katika tuzo hizo na hasa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan kwa kuchangia na kuhamasisha maendeleo ya michezo nchini.
Akizungumza mara baada ya kushinda tuzo hizo, Simbu alisema kuwa amepata faraja kubwa na ushindi huo umemuongezea ari ya kufanya vyema katika mashinadano ya kimataifa ikiwa pamoja na Olimpiki ya mwakani mjini Paris, Ufaransa.
“Nimefarijika sana kwa ushindi huu na umenipa hamasa ya kufanya vyema zaidi katika mashindano mbali mbali ya kimataifa ili kuitangaza nchi yangu. Naipongeza serikali kwa kuandaa tuzo hizo na pongezi za dhati kwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan kwa kuweka hamasa kubwa katika michezo,” alisema Simbu.
Awali, Mwenyekiti wa BMT, Leodegar Tenga alisema kuwa tuzo hizo zitakuwa zinafanyika kila mwaka huku kukiwa na uboreshaji mkubwa kwa lengo la kuleta hamasa nchini hasa kwa wanamichezo chipukizi.
“Huu ni mwanzo tu wa tuzo hizi ambazo tutakuwa tukizifanya kila mwaka huku tukiziboresha. Tunatarajia kuongeza vipengele mbalimbali ikiwa pamoja na kuwapongeza wanamichezo wakongwe walioiletea sifa Tanzania katika michezo mbali mbali limataifa,” alisema Tenga.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa BMT, Neema Msitha alipongeza wadau wote kwa kufanikisha tuzo hizo na kuwaomba kuwaendelea kuwaunga mkoni.
Washindi wengine katika tuzo hizo ni:
Rehema Saidi ambaye alishinda tuzo mbili, ya kwanza ya mwanamichezo bora wa mwaka kwa upande wa tenisi kwa watu wenye ulemavu (Wheel Chair) na tuzo ya mwanamichezo bora wa kike kwa upande wa watu wenye ulemavu.
Wachezaji wengine walioshinda ni Halfani Kianga ambaye ameshinda tuzo ya mchezaji bora wa jumla kwa wanaume kwa upande wa watu wenye ulemavu (amputee).
Madina Idd (gofu wanawake), Fatuma Kibaso (Kriketi wanawake), Evan Ismail (kriketi, wanaume), Yusuph Changalawe (Ngumi ridhaa wanaume), Ibrahim Class (Ngumi za kulipwa), Failuna Matanga( Riadha wanawake), Alphonce Simbu (riadha wanaume), Aishi Manula (soka) wamaume) na Clara Luvanga (soka wanawake.
Washindi wengine ni Collins Saliboko (kuogelea wanaume), Amina Ally mchezaji bora Kabaddi wanawake), Juma Sultan (mchezaju bora wanaume Kabaddi), Raphael Sanga (Michezo ya shule wanaume), Regina Seikali (michezo ya shule wanawake) na Sophia Latiff (Kuogelea wanawake).
Tembo Warriors: Timu bora ya mwaka kwa watu wenye ulemavu, Timu ya taifa ya Kabaddi wanawake, timu bora ya Kabaddi ya taifa wa wanaume, timu ya taifa ya gofu ya wanawake, timu ya Taifa ya wanawake Serengeti Girls, Simba Queens, timu ya kriketi ya wanawake ya chini ya miaka 19, timu ya Taifa ya mchezo wa kuogelea na timu ya Taifa ya wanawake U-17, Serengeti Girls.
Kampuni ya Azam Media Limited nayo ilipewa tuzo maalum kwa mchango wao mkubwa kwenye Sekta ya Michezo, Sanaa na Uatamduni nchini, ambayo ilipokewa na Afisa wake Mwendeshaji Mkuu, Yahya Mohamed.
0 comments:
Post a Comment