TIMU ya Manchester City jana imelazimishwa sare ya 0-0 na wenyeji, FC Copenhagen katika mechi ya utata ya Kundi G Ligi ya Mabingwa Ulaya Uwanja Parken Jijini Copenhagen nchini Denmark.
Teknolojia ya VAR ilitumika mara tatu kipindi cha kwanza kukataa bao la Rodri na kumtoa kwa kadi nyekundu beki Sergio Gomez.
Man City pia ilipewa penalti baada ya Nicolai Boilesen kuunawa mpira, lakini shuti la Riyad Mahrez likaokolewa katika mchezo ambao mshambuliaji wake tegemeo la mabao, Erling Haaland alikuwa benchi muda wote.
Pamoja na sare hiyo, kikosi cha Pep Guardiola kinaendelea kuongoza Kundi kwa pointi zake 10, tatu zaidi ya Borussia Dortmund baada ya wote kucheza mechi nne.
Kwa upande wao, FC Copenhagen wanafikisha pointi mbili sawa na Sevilla wakiendelea kushika mkia kundini.
Ikumbukwe Jumapili mabingwa hao wa England watamenyana na Liverpool katika mchezo wa Ligi Kuu.
0 comments:
Post a Comment