MABONDIA nyota wa Afrika na Marekani watashiriki katika pambano ya Super Dome Boxing yaliyopangwa kufanyika Novemba 4 kwenye ukumbi mpya wa kisasa wa Super Dome Arena.
Mapambano hayo yameandaliwa kwa ushirikiano wa kampuni yenye uzoefu mkubwa wa kuandaa ngumi za kulipwa duniani, Global Boxing Stars kwa ushirikiano na kampuni ya Tanzania, LP Sport chini ya udhamini wa Azam TV kupitia usiku wa Vitasa.
Mabondia ambao watashiriki katika uzinduzi wa Super Dome Boxing ni Nasibu Ramadhani ambaye atazichapa na bondia Toto Helebe wa Afrika Kusini katika uzito wa feather. Pambano hilo limeandaliwa kwa ajili ya kumpromoti bondia Ramadhan kwa mujibu wa promota Levis Paul wa LP Sports.
Paul anaamini kuwa Ramadhan bado ana kipaji cha hali ya juu pamoja na hivi karibuni kutokuwa katika chati ya ngumi hizo kutokana na kukosa mapambano.
“Ramadhan ni bondia mwenye kipajicha hali ya juu tofauti na rekodi zake. Ni bondia ambaye ameweza kupigana katika nchi nyingi duniani na mwenye uzoefu mkubwa. Lengo lengu ni kumrejesha kwenye chati ya hali ya juu na kuwania ubingwa wa kimataifa mwakani,” alisema Levis.
Pambano lingine litakuwa baina ya bondia Shaaban Jongo dhidi ya Mganda, Musa Ntege la kuwania ubingwa wa uzito wa cruiser wa Afrika (ABU) kwa nchi za Afrika Mashariki. Jongo akishinda pambano hilo atapata fursa ya kuwania ubingwa wa Afrika dhidi ya bondia Olanweragu Doradola na kuingizwa katika renki za WBC.
Pambano lingine litakuwa uzito wa juu kati ya bondia Mtanzania anayeishi Sweden Tamim Awadh dhidi ya bondia kutoka Marekani Jarrel Miller ambaye mpaka sasa hajapoteza hata pamban moja kati ya 25 aliyocheza ambapo 21 ameshinda kwa KO na kutoka sare pambano moja. Tamim ameshinda pambano 15 ambapo kati ya hayo, 10 kwa KO na kupoteza matano.
Bondia huyo kwa sasa ni bingwa wa uzito wa juu wa kimataifa wa chama cha World Boxing Foundation (WBF) baada ya kumchapa bondia wa Kosovo, Shkelqim Ademaj katika raundi ya tisa katika mji wa Eissporthalle Essen, Essen, Ujerumani Juni 11 mwaka huu.
“Tunaishukuru timu ya Miller kwa kushirikianana Dimitri Salita, Greg Cohen and LPMG Managament kwa kukubali kuja nchini kushiriki katika pambano hilo. Tunawamba mashabiki wa ngumi za kulipwa kuja kwa wingi kuangalia mapambano hayo,” alisema Jeremy Bean wa Global Boxing Stars.
Bean alisema kuwa mabondia wengine watakaopanda jukwaani siku hiyo ni Mghana, Manyo Plange na Mnigeria Solomon Adebayo ambaye atapambana na Hamis Palasungulu katika uzito wa juu.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Azam TV, Patrick Kahemele alisema kuwa lengo kuu la televisheni yao ni kuendeleza ngumi za kulipwa kimataifa na wanafuraha kubwa kufanya kazi na Global Boxing Stars, LP Sports na ukumbi mpya wa kisasa wa Super Dome.
“Ushirikiano huu utaleta maendeleo makubwa ya ngumi za kulipwa mbali ya kuleta burudani,” alisema Kahemele.
Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Super Dome Tanzania Scott Patrick Farrell alisema kuwa wao ni wa kisasa na lengo kubwa ni kuwa “Las Vegas” ya Afrika Mashariki kwa kuandaa pambano ya ngumi ya kisasa. Farrell alisema kuwa wamepanga kuwa na mapambano manne ya ngumi kila mwaka.
0 comments:
Post a Comment