MABINGWA watetezi, Simba SC wametoa sare ya 1-1 na wenyeji, Azam FC katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara usiku huu Uwanja wa Azam Complex, Chamazi nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Azam FC walitangulia na bao ya mshambuliaji Mzambia, Rodgers Kola dakika ya 37 akimalizia pasi ya chipukizi Sospeter Bajana, kabla ya Nahodha John Raphael Bocco kuisawazishia Simba akiifunga timu yake ya zamani dakika ya 44 kwa pasi ya Shomari Kapombe.
Simba inafikisha pointi 50 baada ya sare ya leo na kuendelea kushika nafasi ya pili ikizidiwa pointi 10 na watani, Yanga baada ya wote kucheza mechi 24.
Azam FC baada ya sare ya leo inafikisha pointi 33, ingawa inabaki nafasi ya tano ikizidiwa pointi moja na Geita Gold na pointi tatu na Namungo FC baada ya wote kucheza mechi 24.
Timu mbili za kwanza zitacheza Ligi ya Mabingwa na mshindi wa tatu atacheza Kombe la Shirikisho Afrika.
Lakini bingwa wa Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC) atatokana na timu tatu za juu, basi na timu itakayomaliza nafasi ya nne itacheza Kombe la Shirikisho Afrika.
0 comments:
Post a Comment