RAIS wa Heshima wa klabu ya Simba, Mohamed ‘Mo’ Dewji amesema bajeti ya uendeshaji ya klabu iliongezeka miaka mitano iliyopita na ndio sababu walifanikiwa kufanya vizuri.
“Miaka mitano iliyopita imekuwa ya mafanikio kwa Simba. Bajeti iliongezeka mara tano, tulishinda makombe mengi ya ndani na tuliweka alama kimataifa kwa kufika robo fainali tatu za michuano ya Afrika,” ameandika Mo Dewji kwenye ukurasa wake wa Instagram.
“Najivunia kuweza kusema tupo katika orodha ya vilabu bora 12 Afrika. Hii imekuwa mara ya kwanza Simba kuwa na mwendelezo mzuri katika miaka 86 ya historia yetu. Hakuna kurudi nyuma, tunatakiwa kufanya mabadiliko katika maeneo ambayo tuna madhaifu na kwenda mbele. Mapambano yanaendelea,” amemalizia.
Msimu huu mambo yamekuwa tofauti Simba SC, kwani licha ya kutolewa mapema Ligi ya Mabingwa Afrika, pia imekwishavuliwa mataji yote, Ngao ya Jamii, Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC) na Ligi Kuu ambako watani wao, Yanga wanahitaji kushinda mechi moja zaidi kutawazwa mabingwa.
Simba ambayo taji pekee ililotwaa msimu huu ni Kombe la Mapinduzi Januari mwaka huu Zanzibar, baada ya kutolewa Ligi ya Mabingwa iliangukia Kombe la Shirikisho Afrika ambako nako ilitolewa katika Robo Fainali.
0 comments:
Post a Comment