MABINGWA wa Tanzania, Simba SC wamefanikiwa kwenda Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya ushindi wa 4-0 dhidi ya US Gendamarie ya Niger usiku huu Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.
Mabao ya Simba inayofundishwa na kocha Mspaniola, Pablo Franco Martin yamefungwa na kiungo Mmali, Sadio Kanouté dakika ya 63, mshambuliaji Mkongo Chris Kope Mutshimba Mugalu dakika ya 68 na 78 na kipa Saidu Hamisu aliyejifunga dakika ya 84 katika harakati za kuokoa.
Sifa zimuendee winga Mghana, Bernard Morrison aliyeseti mabao mawili ya kwanza baada ya dakika 45 ngumu za kipindi cha kwanza.
Simba inamaliza na pointi 10, sawa na RSB Berkane wakilingana hadi wastani wa mabao na zote zinakwenda Nane Bora zikizipiku ASEC Mimosas ya Ivory Coast iliyomaliza na pointi tisa na Gendamarie pointi tano.
RSB Berkane wamefuzu baada ya ushindi wa nyumbani wa 1-0 dhidi ya ASEC leo Uwanja wa Manispaa y Berkane nchini Morocco.
Timu nyingine zilizokwenda Robo Fainali ni Al Ahli Tripoli ya Libya na Pyramids ya Misri kutoka Kundi A, Orlando Pirates ya Afrika Kusini na Al-Ittihad ya Libya Kundi B, TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Al Masry ya Misri Kundi C.
Droo ya Robo Fainali itapangw Aprili 5, mwaka huu makao makuu ya Shirikisho (CAF), Jijini Cairo, nchini Misri.
0 comments:
Post a Comment