Kwa mara nyingine, utamu wa mechi ulikuwa baina ya Wakongo, beki Henock Inonga Baka ‘Varane’ wa Simba na mshambuliaji, Fiston Kalala Mayele wa Yanga namna ambavyo wamepambana leo uwanjani.
Kama ilivyokuwa kwenye mechi ya kwanza ya ligi, Inonga alimdhibti vyema Mayele, kinara wa mabao Ligi Kuu ambaye muda wote wa mchezo alipiga shuti moja tu lililogonga nyavu za pembeni, nje kulia kipindi cha pili.
Simba pekee waliofanya jaribio la hatari lililolenga lango, Mkongo mwingine, mshambuliaji Chris Kope Mutshimba Mugalu alipounganishia mikononi mwa kipa Djigui Diarra mpira wa adhabu wa beki Shomari Kapombe kipindi cha pili pia.
Zaidi ya hapo mechi ilikuwa ya kukamiana na kuonyeshana ubabe baina ya wachezaji wa pande zote mbili na pongezi kwa refa chipukizi, Ramadhani Kayoko kwa kuimudu pamoja na makosa machache ya kibinadam aliyoyafanya.
Kwa sare hiyo, Simba wanafikisha pointi 42 baada ya mechi 20, wakizidiwa pointi 13 na watani wao wa jadi, Yanga ambao hata hivyo wamecheza mechi moja zaidi.
Watani hao wa jadi wanaweza kukutana tena kabla msimu kufungwa katika mechi ya Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC), iwapo Simba wataitoa Pamba FC ya Mwanza.
0 comments:
Post a Comment