WAZIRI wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa amesema kuwa kuanzishwa kwa Mfuko wa Maendeleo ya Michezo na kutengwa kwa asilimia tano ya fedha za Bahati Nasibu kumesaidia maendeleo ya michezo nchini.
Kauli hiyo imetolewa Machi 16, 2022 Mji wa Serikali-Mtumba Jijini Dodoma Waziri Mchengerwa alipokuwa akieleza mafanikio ya wizara yake kwa kipindi cha mwaka mmoja madarakani mwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.
“Hadi Februari mwaka huu kiasi cha TZS Bilioni 1.55 kimepokelewa kutoka Hazina. Fedha hizi zimeanza kusaidia maendeleo mbalimbali ya michezo nchini na zitasaidia pia katika programu za uendelezaji wa miundombinu.”
Sambamba na hilo Mheshimiwa Mchengerwa alibainisha kuwa katika mwaka mmoja huu, serikali imekamilisha hatua muhimu za ujenzi wa miundombinu ya michezo ikiwemo kukamilika usanifu wa uwanja wa soka wa Dodoma, kukamilika usanifu wa ujenzi wa viwanja vya mazoezi na kupumzikia wananchi vitakavyojengwa Dar es Salaam, Dodoma na Geita.
Akiyataja mafanikio mengine ya wizara hii alisema kuwa jumla ya TZS Bilioni 19 zitatumika kukarabati shule 58 za michezo na kuwekewa miundombinu mbalimbali ya kisasa.
Waziri Mchengerwa alisema kuwa nchi ya Tanzania, Novemba mwaka 2021 ilipata bahati ya kuwa mwenyeji wa Mashindano ya Soka kwa Walemavu Afrika (CANAF-2021) ambapo pamoja na kupokea takribani nchi 13 kutoka Afrika, Timu ya Taifa ya Tanzania ya Soka la Walemavu, Tembo Warriors, ilikuwa miongoni mwa Timu nne zilizofuzu kutoka Afrika kwenda Kombe la Dunia Uturuki Oktoba mwaka huu.
0 comments:
Post a Comment