WENYEJI, Yanga SC wamelazimishwa sare ya bila kufungana na Mbeya City katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara usiku wa leo Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.
Sare inayoiongezea alama moja kila timu, inaifanya Yanga ifikishe pointi 36 na kuendelea kuongoza ligi kwa pointi nane zaidi ya mabingwa watetezi, Simba SC baada ya wote kucheza mechi 14.
Mbeya City yenyewe inafikisha pointi 23 katika mchezo wa 14, ingawa inabaki nafasi ya tatu ikizidiwa pointi moja na Azam FC.
Mechi nyingine ya Ligi Kuu leo, Kagera Sugar imeibuka na ushindi wa 2-1 dhidi ya Coastal Union Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
Mabao ya Kagera Sugar yamefungwa na Erick Mwijage dakika ya 20 na 73, wakati la Coastal Union limefungwa na Vincent Abubakar dakika ya 54.
Kagera Sugar inafikisha pointi 19 na kusogea nafasi ya tano, wakati Coastal Union inabaki na pointi zake 17 katika nafasi ya nane baada ya wote kucheza mechi 14.
Nayo KMC imelazimishwa sare ya 1-1 na Biashara United Uwanja wa Azam Complex, Chamazi nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
KMC inafikisha pointi 16 katika nafasi ya 10 na Biashara United inafikisha pointi 12 katika nafasi ya 13 kwenye ligi ya timu 16 baada ya timu zote kucheza mechi 14.
0 comments:
Post a Comment