VIGOGO, Yanga SC wamefanikiwa kwenda Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC) baada ya ushindi wa 2-1 dhidi ya Biashara United usiku huu Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.
Mabao ya Yanga SC yote leo yamefungwa na nyota wake kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), beki Yannick Litombo Bangala dakika ya 22 na mshambuliaji Fiston Kalala Mayele dakika ya 28, wakati la Biashara United limefungwa na mshambuliaji Mkenya, Collins Opare dakika ya 38.
Katika mchezo uliotangulia, Polisi Tanzania ilifanikiwa pia kwenda Robo Fainali ya ASFC baada ya ushindi wa 2-0 dhidi ya wenyeji, Tanzania Prisons mabao ya Said Khamis dakika ya 40 na Daruwesh Saliboko dakika ya 83 Uwanja wa Sokoine Jijini Mbeya.
Timu nyingine zilizofuzu Robo Fainali ni Azam FC iliyoichapa Baga Friends 6-0, Geita Gold iliyoichapa Mbuni FC 1-0, Coastal Union iliyoichapa Mtibwa Sugar 2-0 na Kagera Sugar iliyoilaza Namungo FC 1-0.
Hatua ya 16 Bora ya ASFC itakamilishwa kesho kwa michezo mingine miwili, Pamba na Dodoma Jijini Mwanza na Ruvu Shooting dhidi ya mabingwa watetezi, Simba SC Jijini Dar es Salaam.
0 comments:
Post a Comment