TIMU ya taifa ya Senegal imefanikiwa kutwaa ubingwa wa Kombe la Mataifa ya Afrika kwa mara ya kwanza katika historia yake baada ya ushindi wa penalti 4-2 kufuatia sare ya bila kufungana na Misri ndani ya dakika 120 usiku huu Uwanja wa Paul Biya Jijini Yaoundé nchini Cameroon.
Shujaa wa Simba wa Teranga ni kipa wa Chelsea ya England, Édouard Mendy aliyeokoa mkwaju wa penalti wa nne wa Mafarao uliopigwa na Mohanad Lasheen baada ya awali, Mohamed Abdelmonem kugongesha mwamba shuti lake.
Waliofunga penalti za Misri ni Ahmed Mostafa Mohamed Sayed 'Zizo' na Marwan Hamdy pekee.
Upande wa Senegal waliofunga ni Kalidou Koulibaly, Abdou-Lakhad Diallo, Cheikh Ahmadou Bamba Mbacke Dieng na Sadio Mane, wakati mkwaju wa Bouna Junior Sarr uliokolewa na kipa Mohamed Abou Gabal 'Gabaski '.
Mapema tu katika dakika ya tatu mchezo, Senegal walipata penalti baada ya Mohamed Abdelmonem kumuangusha kwenye boksi beki mwenzake, Saliou Ciss lakini Gabaski akaokoa mkwaju wa Mane baada ya kupewa maelekezo na Nahodha wake, Mohamed Salah.
Salah na Mane wote wanacheza Liverpool na hilo linakuwa taji la kwanza la AFCON kwa Senegal katika fainali ya tatu baada ya mwaka 2002 na 2019.
0 comments:
Post a Comment