WENYEJI, Namungo FC wameibuka na ushindi wa 3-1 dhidi ya Mtibwa Sugar katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa mkoani Lindi.
Mabao ya Namungo FC yamefungwa na Ibrahim Mkoko dakika ya 33 na Relliant Lusajo mawili, dakika ya 18 na 52, wakati la Mtibwa limefungwa na Muludi Mayanja dakika ya 45 na ushei.
Kwa ushindi huo, Namungo inafikisha pointi 20 na kusogea nafasi ya tano, wakati Mtibwa inabaki na pointi zake 12 katika nafasi ya 14 kwenye ligi ya timu 16 baada ya wote kucheza mechi 14.
Nayo Geita Gold imetumia vyema Uwanja wa nyumbani, Nyankumbu kwa kuichapa Polisi Tanzania 3-1.
Mabao ya Geita yamefungwa na Kelvin Nashon dakika ya 20, George Mpole dakika ya 24 na Amos Charles dakika ya 46, wakati la Polisi limefungwa na Vitalis Mayanga dakika ya 70.
Kwa ushindi huo, Geita inafikisha pointi 17 na kusogea nafasi ya nane, wakati Polisi inabaki na pointi zake 18 na kuteremka kwa nafasi moja hadi ya saba baada ya wote kucheza mechi 14.
Ikumbukwe mwisho wa msimu timu mbili zitateremka moja kwa moja na mbili zitamenyana na timu za Championship kuwania kubaki Ligi Kuu.
0 comments:
Post a Comment