VINARA, Yanga SC wameendelea kuwapa raha mashabiki wao baada ya ushindi wa 1-0 dhidi ya wenyeji, wahamiaji Polisi Tanzania katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Jijini Arusha.
Bao pekee la Yanga jioni ya leo limefungwa kiungo mshambuliaji, Dickson Ambundo aliye katika msimu wa kwanza baada ya kusajiliwa kutoka Dodoma Jiji FC ambaye alimalizia kazi nzuri ya mshambuliaji Mkongo, Fiston Kalala dakika ya 64.
Kwa ushindi huo, Yanga SC inafikisha pointi 35 katika mchezo wa 13 na kuendelea kuongoza ligi kwa pointi 10 zaidi ya mabingwa watetezi, Simba SC ambao hata hivyo wana mechi moja mkononi.
Polisi Tanzania wanabaki na pointi zao 18 za mechi 13 sasa katika nafasi ya tano.
Mechi nyingine ya Ligi Kuu leo, Namungo FC imeibuka na ushindi wa 3-1 dhidi ya wenyeji, Coastal Union Uwanja wa Mkwakwani Jijini Tanga.
Mabao ya Namungo FC yamefungwa na washambuliaji Mzambia Obrey Chirwa dakika ya 38 na mzawa, Relliant Lusajo mawili dakika ya 81 na 85, wakati bao pekee la Coastal alijifunga Abdulmik Zacharia dakika ya 46.
Namungo inafikisha pointi 17 katika mchezo wa 13 na kusogea nafasi ya sita, ikiishushia Coastal nafasi ya saba ambayo inabaki a pointi zake 17 za mechi 13 pia.
0 comments:
Post a Comment