WENYEJI, Cameroon wamefanikiwa kwenda Robo Fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika baada ya ushindi wa 2-1 dhidi ya Comoro usiku wa Jumatatu Uwanja wa Paul Biya Jijini Yaoundé.
Mabao ya Cameroon yamefungwa na Karl Toko Ekambi dakika ya 29 na Vincent Aboubakar dakika ya 70, wakati la Comoro limefungwa na Youssouf M'Changama dakika ya 81.
Comoro ilipata pigo la mapema kufuatia kiungo wake, Jimmy Abdou kutolewa kwa kadi nyekundu ya moja kwa moja dakika ya sita.
Comoro iliingia kwenye mchezo huo bila wachezaji wake nyota 12 kwa sababu ya majeruhi na kukutwa na virusi vya corona, wakiwemo makipa wote watatu, ambao ni Salim Ben Boina majeruhi, wakati Ali Ahamada na Moyadh Ousseini wana COVID.
Lakini beki wa kushoto wa Ajaccio ya Ligie 2 Ufaransa, Chaker Alhadhur aliyesimama langoni alifanya kazi nzuri mno.
Katika mchezo uliotangulia, Gambia iliitupa nje Guinea kwa kuichapa 1-0, bao pekee la mshambuliaji wa Bologna ya Italia, Musa Barrow dakika ya 71 Uwanja wa Bafoussam.
Sasa Cameroon itakutana na Gambia katika Robo Fainali Jijini Douala Jumamosi.
0 comments:
Post a Comment