BAO pekee la winga Mkongo, Jesus Ducapel Moloko limeendeleza furaha kwa mashabiki wa Yanga SC baada ya ushindi wa 1-0 dhidi ya Geita Gold Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.
Moloko aliyejiunga na Yanga msimu huu kutoka AS Vita ya kwao, Kinshasa alifunga bao hilo dakika ya 17 kwa shuti la mguu wa kulia akimalizia pasi nzuri ya mshambuliaji Mburkinabe, Yacouba Sogne baada ya kuwatoka kwa ustadi mabeki wa Geita.
Yanga inafikisha pointi sita baada ya mechi mbili, ikiwa ni muendelezo wa ushindi wa 1-0 kuanzia dhidi ya Simba kwenye Ngao ya Jamii na mechi ya kwanza ya ligi dhidi ya Kagera Sugar mjini Bukoba.
Mechi nyingine za Ligi Kuu leo, wenyeji Polisi Tanzania wameibuka na ushindi wa 2-1 dhidi ya Azam FC Uwanja wa Ushirika mjini Moshi mkoani Kilimanjaro.
Mabao ya Polisi leo yamefungwa na Kassim Shaaban dakika ya 23 na Adam Adam dakika ya 40, wakati la Azam FC limefungwa na Iddi Suleiman 'Nado'.
Ni ushindi wa pili kwa Maafande wa Jeshi la Usalama wa Raia baada ya kuichapa KMC 2-0 kwenye mechi ya kwanza Karatu, wakati Azam FC wanafikisha mechi mbili bila ushindi, kufuatia kutoa sare ya 1-1 na Coastal Union Jijini Tanga.
Nayo Coastal Union imetoa sare ya pili mfululizo nyumbani, 0-0 na KMC Uwanja wa Mkwawani, Tanga.
0 comments:
Post a Comment