ALIYEKUWA Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa klabu ya Simba, Haji Sunday Manara leo amejiunga na mahasimu wa jadi, Yanga SC.
Manara ametambulishwa leo katika mkutano na Waandishi wa Habari hoteli ya Serena Jijini Dar es Salaam kuelekea tamasha la kila mwaka la Yanga la kilele cha Wiki ya Mwananchi Jumapili Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.
Manara alijiuzulu Simba SC mwezi uliopita baada ya kutofautiana na Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Barbara Gonzalez aliyemtuhumu kuihujumu klabu hiyo kwa Yanga.
Hayo yalitokea siku chache kabla ya Fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC) baina ya timu hizo Julai 3 ambayo Simba ilishinda 1-0 Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma.
Na Manara anakuwa Afisa wa pili wa Simba kujiunga na Yanga ndani ya mwaka mmoja baada ya aliyekuwa Mtendaji Mkuu kabla ya Barbara, Senzo Mazingisa Mbatha, raia wa Afrika Kusini ambaye amepewa cheo cha Ushauri wa klabu ya Jangwani.
Manara ni mtoto wa mchezaji wa Yanga miaka ya 1970, Sunday Manara ambaye kaka yake, Kitwana na mdogo wake Kassim pia walicheza klabu hiyo.
Na Manara alizaliwa wakati baba yake anacheza Yanga na wakati huo alikuwa nyota mkubwa wa timu ya Jangwani kiasi cha kupewa jina la utani, Computer kabla ya kwenda Uholanzi kucheza soka ya kulipwa baadaye Marekani, Austria na Qatar.
0 comments:
Post a Comment