RASMI, Simba SC ni mabingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara kwa msimu wa nne mfululizo baada ya ushindi wa 2-0 dhidi ya Coastal Union ya Tanga usiku huu Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.
Mabao ya Simba SC leo yamefungwa na washambuliaji, Nahodha John Raphael Bocco dakika ya 14 na Mkongo, Chris Kope Mutshimba Mugalu dakika ya 23.
Simba SC imefikisha pointi 79 baada ya mechi 32, tisa zaidi ya watani wao wa jadi, Yanga SC kuelekea mechi mbili za mwisho za msimu, maana yake hata wakipoteza michezo hiyo hawawezi kufikiwa.
Hilo ni taji la nne mfululizo na la 22 jumla, sasa wanahitaji kutwaa mataji matano zaidi ili kuwafikia Yanga idadi ya kubeba ubingwa wa nchi, ambao wanaongoza baada ya kuchukua mara 27.
Kwa kubeba taji hilo kwa mara ya nne leo (2018, 2019, 2020 na 2021), Simba sasa inaongoza kutwaa taji la ligi kuu zaidi ya mara tatu, hii ikiwa ni mara ya pili baada ya kulibeba mfululizo 1976, 1977, 1978, 1979 na 1980.
Watani wao wa jadi, Yanga ndio waliokuwa wa kwanza kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu ya Bara zaidi ya mara tatu, 1968, 1969, 1970, 1971 na 1972.
Pamoja na kujivunia kulitwaa mara nyingi zaidi taji hilo (27), Yanga pia ndio timu inayoongoza kutwaa ubingwa wa Bara zaidi ya mara mbili – ikiwa imefanya hivyo mara nne jumla ikiwemo ya miaka mitano mfululizo, wakati Simba hii inakuwa mara ya pili kubeba taji hilo zaidi ya mara mbili.
Timu nyingine zilizotwaa taji hilo ni Cosmopolitans ya Dar es Salaam 1967, Mseto SC ya Morogoro 1975, Pan African ya Dar es Salaam 1982, Tukuyu Stars ya Mbeya 1986, Coastal Union ya Tanga 1988, Mtibwa Sugar ya Morogoro 1999 na 2000 na Azam FC ya Dar es Salaam pia 2014.
0 comments:
Post a Comment