SIMBA SC imefanikiwa kwenda Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya ushindi wa 4-1 dhidi ya AS Vita Club ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) katika mchezo wa Kundi A jioni ya leo Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.
Mabao ya Simba SC leo yamefungwa na viungo Luis Miquissone kutoka Msumbiji dakika ya 30 na Wazambia Clatous Chama dakika ya 45 na ushei na 84 na Larry Bwalya dakika ya 66, wakati bao pekee la Vita limefungwa na kiungo Mkongo Zemanga Soze dakika ya 32.
Kwa ushindi huo, Simba SC inayofundishwa na Mfaransa Didier Gomes Da Rosa inafikisha pointi 13 na kuendelea kuongoza kundi hilo, ikifuatiwa na mabingwa watetezi, Al Ahly ya Misri yenye pointi nane.
Baada ya sare ya 2-2 na wenyeji, El Merreikh nchini Sudan leo, Ahly inamaliza nafasi ya pili na kuungana na Simba SC kwenda Robo Fainali.
Kuelekea mechi za mwisho Aprili 9, AS Vita ina pointi nne na Merreikh pointi mbili wote wakiwa wameaga mashindano.
Simba SC iliyoruhusu bao la kwanza leo kwenye kundi lake katika mechi tano itamaliza na Al Ahly Jijini Cairo na As Vita na Merreikh Jijini Kinshasa.
0 comments:
Post a Comment