TIMU ya Azam FC imelazimishwa sare ya 2-2 na wenyeji, Dodoma Jiji FC katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara Uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma.
Mabao ya Azam FC yamefungwa na Mzimbabwe Prince Dube Mpumelelo dakika ya pili na Mzambia Obrey Choro Chirwa dakika ya 90 na ushei, wakati ya Dodoma Jiji FC yamefungwa na Seif Abdallah Karihe dakika ya 71 na Anuary Jabir dakika ya 77.
Kwa matokeo hayo, Azam FC inafikisha pointi 51 baada ya kucheza mechi 27 na kuendelea kushika nafasi ya tatu, nyuma ya mabingwa watetezi, Simba SC wenye pointi 55 za mechi 23 na Yanga SC wenye pointi 57 za mechi 26.
Dodoma Jiji yenyewe sasa hivi ina pointi 38 baada ya kucheza mechi 27 na imepanda nafasi ya sita kutoka ya saba.
Mechi iliyotangulia leo mchana, Ihefu SC imeichapa Tanzania Prisons 1-0, bao pekee la kiungo Raphael Daudi Lothi dakika ya sita Uwanja wa Highland Estate, Ubaruku, Mbaraki mkoani Mbeya.
Ihefu SC inafikisha pointi 27 baada ya kucheza mechi 27 na kupanda kwa nafasi moja hadi ya 16 katika ligi ya timu 18, ambayo mwishoni mwa msimu timu nne zitashuka daraja moja kwa moja na mbili kwenda kucheza na timu za Daraja la Kwanza kuwania kubaki Ligi Kuu.
Tanzania Prisons kwa sasa ni ya nane ikiwa na pointi 34 za mechi 26.
0 comments:
Post a Comment