Na Anitha Jonas – WHUSM, DODOMA
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli amemwagiza Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Innocent Bashungwa kuhakikisha anaunda timu ya soka ya tifa isiyohusisha klabu kongwe nchini, Simba na Yanga.
Rais Magufuli ametoa agizo hilo leo Desemba 09, 2020 Ikulu Chamwino Jijini Dodoma wakati wa hafla ya kuwaapisha Mawaziri aliyowateuwa hivi karibuni mara baada ya kuundwa kwa Serikali Awamu ya Tano Muhula wa Pili katika baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.
“Bashungwa tumekupeleka kwenye michezo tunataka tushinde, sio tukilala tukiamka mabao kumi, wote mtaondoka wewe na Naibu Waziri wako, wakati sasa umefika tuondokane na Usimba na Yanga umetuchelewesha sana, sisi tunataka kushinda na michezo iweze na matokeo na itoe ajira”alisema Dkt. Magufuli.
Akiendelea kuzungumza katika hafla hiyo Rais Magufuli aliwasisitiza Mawaziri hao kusimamia suala la Wasanii kukosa haki zao.
Mara baada ya kuapishwa Waziri Bashungwa na Naibu wake Abdallah Ulega waliripoti moja kwa moja katika Ofisi za Wizara zilizopo Mtaa wa Habari Mji wa Serikali Mtumba ambapo walipokelewa na watumishi na kuzungumza Menejimenti ya wizara hiyo.
Katika kikao chake na Menetimenti, Waziri Bashungwa alitoa maelekezo kwa Idara ya Maendeleo ya Michezo kuandaa mpango mkakati wa kutekeleza Sera ya Michezo na kuuwasilisha ofisini kwake ifikapo Desemba 31, 2020, pamoja na kuhakikisha wizara inatimiza ndoto za wadau wa sekta zake.
“Ahadi nyingi za Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli zinapitia kwenye wizara hii, tumsaidie Mheshimiwa Rais kutekeleza ahadi alizotoa wakati wa kampeni ikiwemo suala la kuendeleza sekta ya Sanaa na Michezo nchini,”alisema Bashungwa.
Halikadhalika nae Naibu Waziri Ulega alisema kuwa wizara hiyo ni moja ya eneo linalotengeneza ajira kwa vijana kupitia sekta za Habari, Sanaa na Michezo, na kuwataka Wakuu wa Idara waongeze ubunifu na kuweka mikakati endelevu ya kusimamia sekta hizo ili kutimiza maono ya Rais kwa wananchi wake.
“Rais ametuamini, tutamsaidia kutekeleza maono yake pamoja na yale yaliyoainishwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020 katika kuwaletea maendeleo wananchi,”alisema Ulega.
Aidha, viongozi hao wamemshukuru Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuwateuwa ili kusimamia wizara hiyo ambayo ni nguvu laini ya nchi ‘soft power’ yenye dhamana ya kusimamia tunu za taifa ikiwemo Amani, Umoja, Upendo na Mshikamano.
Mara baada ya kuwapokea viongozi hao katika ofisi za Wizara, Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi amewapongeza Waziri na Naibu Waziri kwa kuteuliwa na Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli kusimamia Wizara hiyo na amewaahidi kuwa Menejimenti pamoja na watumishi wote watawapa ushirikiano ili waweze kutimiza majukumu kufikia azzma ya Serikali ya kuwatumikia wananchi katika sekta za Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
0 comments:
Post a Comment