Na Mwandishi Wetu, BUKOBA
VIGOGO, Yanga SC wamewaangusha wenyeji, Kagera Sugar kwa kuwachapa 1-0 katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
Kwa ushindi huo, Yanga SC inayofundishwa na kocha Mserbia, Zlatko Krmpotic inafikisha pointi saba baada ya mechi tatu, ikishinda mbili na sare moja katika mechi zake mbili za awali nyumbani, Dar es Salaam.
Kwenye mchezo huo uliochezeshwa na refa Hussein Hamisi wa Katavi aliyesaidiwa na Joseph Masija wa Mwanza na Robart Rwemeja wa Mara, bao pekee la Yanga SC limefungwa na kiungo kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Serge Mukoko Tonombe.
Serge Mukoko Tonombe akikimbia kushangilia baada ya kuifungia Yanga SC bao pekee leo Uwanja wa Kaitaba
Tonombe alifunga bao hilo dakika ya 73 baada ya kutuliza vizuri mpra kwenye boksi na kumchambua kipa Issa Chalamanda kwa shuti la juu kufuatia pasi ya mchezaji mwenzake wa zamani wa AS Vita ya Kinshasa, kwao DRC.
Bao hilo lilibadili mfumo wa mchezo wa kujihami wa Kagra Sugar tangu mwanzoni mwa mchezo na wao kuanza kwenda kushambulia moja kwa moja, hivyo kuongeza ladha ya mechi hiyo.
Lakini bahati ilikuwa kwa Yanga SC leo waliofanikiwa kujilinda vizuri na kumalizia vyema mchezo huo wakiondoka na pointi zote tatu dhidi ya timu ya mzalendo, kocha Mecky Mexime.
Mchezo uliotangulia leo mchana, Tanzania Prisons ilipata ushindi wa kwanza baada ya kuwachapa Namungo FC 1-0, bao pekee la Gasper Mwaipasi dakika ya 47 Uwanja wa Nelson Mandela, Sumbawanga mkoani Rukwa.
Prisons wanafikisha pointi nne baada ya mechi tatu, kufuatia kufungwa na kutoa sare mechi mbili za awali ugenini, wakati Namungo FC, wawakilishi wa Tanzania kwenye Kombe la Shirikisho msimu huu – wanabaki na pointi zao tatu kufuatia kufungwa mechi nyingine moja nyumbani na kushinda moja.
Raundi ya tatu ya Ligi Kuu itaendelea kesho kwa mechi tatu, mabingwa watetezi, Simba SC wakimenyana na Biashara United ya Mara na Coastal Union wakiikaribisha Dodoma Jiji Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, wakati Mbeya City watamenyana na Azam FC Uwanja wa Sokoine Jijini Mbeya.
Raundi ya tatu itakamilishwa Jumatatu kwa michezo mingine miwili, Ruvu Shooting na Gwambina Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani na Mwadui FC watawakaribisha KMC Uwanja wa Mwadui Complex, Shinyanga.
Kikosi cha Kagera Sugar kilikuwa; Ramadhani Chalamanda, Mwaita Gereza, Davd Luhende, Ally Mtoni ‘Sonso’, Erick Kyaruzi, Ally Nassor ‘Ufudu’, Ally Ramadhani, Abdallah Seseme/Mbaraka Yussuph dk79, Hassan Mwaterema/ Nassoro Kapama dk87, Mohamed Ibrahm ‘Mo’/Eric Mwijage dk36 na Vitalis Mayanga.
Yanga SC; Metacha Mnata, Kibwana Shomari/Deus Kaseke dk57, Yassin Mustapha, Lamine Moro, Bakari Mwamnyeto, Mukoko Tonombe, Zawadi Mauya/Harouna Niyonzima dk80, Feisal Salum ‘Fei Toto’, Michael Sarpong, Yacouba Sogne/Carlos Calinhos dk57 na Tuisila Kisinda.
0 comments:
Post a Comment