Na Mwandishi Wetu, CAIRO
OFISA Mtendaji Mkuu wa Simba SC, Barbara Gonzalez amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF), Ahmad Ahmad kwenye makao makuu ya shirikisho hilo Jijini Cairo, Misri.
Baada ya kukutana Rais Ahmad amempongeza Barbara kwa kupata nafasi hiyo kubwa, lakini pia kumtaka kuitumia vyema ili kuonesha kwamba anaimudu kazi hiyo ambapo itakuwa ni moja ya njia ya kuhamasisha wanawake wengine kushika nafasi za juu za uongozi wa soka.
Kwa upande wake Barbara amemshukuru Rais Ahmad na CAF kwa mapokezi mazuri, lakini pia kuahidi kufanya kazi kwa bidii ili kusaidia kukuza soka la Afrika.
Wengine waliohudhuria kikao hicho ni Katibu Mkuu wa CAF, Abdelmounaïm Bah, Makamu Katibu Mkuu wa CAF, Anthony Baffoe na Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi, Mulamu Nghambi.
Awali ya hapo, Barbara Gonzalez alitembelea makao makuu ya klabu kongwe za Misri, Al Ahly na Zamalek na kukubaliana kushirikiana nazo katika mambo mbalimbali.
Barbara alisema wamekubalina na Al Ahly kushirikiana kwenye maeneo ya biashara, ufundi na uendelezaji wa wachezaji kwa kujenga kituo cha kukuza vipaji nje ya Misri, hapa Afrika ambacho kitaendeshwa na klabu hizo.
Barbara aliongeza kwamba pia wamekubaliana na Al Ahly baadae ije nchini kucheza mchezo wa kirafiki na Simba SC.
0 comments:
Post a Comment