WENYEJI, Simba SC wamefanikiwa kutinga hatua ya 16 Bora Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC) baada ya ushindi wa 2-1 dhidi ya Mwadui FC ya Shinyanga jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Ushindi huo kwa Simba SC ni sawa na kulipa kisasi baada ya kuchapwa 1-0 na Mwadui FC, lakini mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara Jumatano ya Oktoba 30, mwaka jana Uwanja wa Kambarage, Shinyanga bao pekee la Gerald Mathias Mdamu.
Na haukuwa ushindi mwepesi kwa Simba SC, kwani na leo walitanguliwa kwa mara nyingine Gerald Mathias Mdamu akiwatungua dakika ya 34 akimalizia krosi nzur Venance Ludovic, aliyemtoka kiungo Mkenya, Francis Kahata upande wa kulia.
Simba SC inayofundishwa na kocha Mbelgiji, Sven Ludwig Vandonbroeck ikafanikiwa kusawazisha dakika ya 45 na ushei kwa bao la kiungo Mzambia, Clatous Chota Chama baada ya kuwatoka mabeki wa Mwadui FC kufuatia pasi ya kiungo wa kimataifa wa Tanzania, Hassan Dilunga.
Kipindi cha pili timu zote zilirejea kwa tahadhari, zikishambulia kwa tahadhari na kujilinda zaidi, lakini zikiwa zimesalia dakika tano mchezo kumalizika, Kahata akasahihisha makosa yake kwa kuifungia Simba SC bao la ushindi kwa kichwa akimalizia krosi ya beki wa kulia, Shomari Kapombe.
Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Beno Kakolanya, Shomari Kapombe, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’/Gardiel Michael dk90+1, Erasto Nyoni, Pascal Wawa, Jonas Mkude, Hassan Dilunga/John Bocco dk87, Sharaf Shiboub/Ibrahim Ajibu dk71, Meddie Kagere, Clatous Chama na Francis Kahata.
Mwadui FC; Mussa Mbissa, Mfaume Omary, Khalfan Mbarouk, Augustino Samson, Joram Mgeveke, Erick Nkosi, Benjamin Sowah/Malick Jaffar dk79, Charles Ndahaza, Gerald Mathias/Abdul Maskini dk58, Ludovic Evans na Omar Daga.
0 comments:
Post a Comment