// Disable text selection (not fully reliable) function disableSelection(element) { element.setAttribute('unselectable', 'on'); element.style.userSelect = 'none'; element.style.MozUserSelect = 'none'; element.style.webkitUserSelect = 'none'; } // Apply to the entire document body document.addEventListener('DOMContentLoaded', function() { disableSelection(document.body); }); HONGERA SIMBA SC, KAFANYIENI KAZI MAPUNGUFU YALIYOONEKANA - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE HONGERA SIMBA SC, KAFANYIENI KAZI MAPUNGUFU YALIYOONEKANA - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE
  • HABARI MPYA

    Sunday, April 14, 2019

    HONGERA SIMBA SC, KAFANYIENI KAZI MAPUNGUFU YALIYOONEKANA

    SAFARI ya Simba SC katika Ligi ya Mabingwa Afrika ilifikia tamati jana baada ya kuchapwa mabao 4-1 na wenyeji, Tout Puissant Mazembe katika mchezo wa marudiano wa Robo Fainali Uwanja wa Mazembe mjini Lubumbashi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
    Kwa matokeo hayo Simba SC imetolewa kwa jumla ya mabao 4-1 baada ya sare ya 0-0 kwenye mchezo wa kwanza Jumamosi ya wiki iliyopita mjini Dar es Salaam, hivyo kushindwa kurudia rekodi yake ya mwaka 1974 kufika Nusu Fainali.  
    Katika mcheze huo uliochezeshwa na refa Janny Sikazwe, aliyesaidiwa na Romeo Kasengele wote wa Zambia na Berhe Tesfagiorgis O'michael wa Eritrea, hadi mapumziko TP Mazembe walikuwa mbele kwa mabao 2-1.

    Lakini ni Simba SC waliokuwa wa kwanza kupata bao dakika ya pili tu kupitia kwa mshambuliaji wake wa kimataifa wa Uganda, Emmanuel Arnold Okwi aliyemlamba chenga kipa Muivory Coast, Sylvain Gbohouo baada ya pasi ya kiungo Mnyarwanda, Haruna Niyonzima na kufunga kiulaini.
    Mazembe ikasawazisha bao hilo dakika ya 23 kupitia kwa beki wake Mzambia Kabaso Chongo aliyemalizia pasi ya mshambuliaji Jackson Muleka baada ya kona iliyochongwa na Tressor Mputu.
    Na Meschak Elia akaifungia Mazembe bao la pili dakika ya 38 kwa shuti la mguu wa kushoto akitumia makosa ya beki Mburkinabe wa Simba SC, Zana Coulibaly.
    Kipindi cha pili, kocha Mbelgiji wa Simba SC, Patrick Aussems akaanza na mabadiliko mfululizo akiwatoa beki Mganda Juuko Murshid na kiungo Muzamil Yassin na kuwaingiza kiungo Mzambia Clatous Chama na mshambuliaji Mnyarwanda, Meddie Kagere.
    Hayakuwa mabadiliko yenye manufaa kwa timu, kwani yaliwasaidia Mazembe kupata mabao mawili zaidi, wafungaji Tessor Mputu dakika ya 62 na Muleka dakika ya 75, huku kipa Aishi Salum Manula akifanya kazi ya ziada kuokoa michomo zaidi ya hatari.
    Simba SC inarejea Dar es Salaam usiku wa leo kuelekeza nguvu zake kwenye Ligi Kuu ya Tanzania Bara ili iweze kutetea taji lake na kupata tena nafasi ya kucheza michuano ya Afrika msimu ujao. 
    Simba SC itajilaumu yenyewe kwa kutobuka na ushindi kwenye mechi ya kwanza Jumamosi ya wiki iliyopita licha ya kucheza vizuri mno na kuihimili TP Mazembe, mabingwa mara nne wa Ligi ya Mabingwa Afrika.    
    Siku hiyo, dakika ya 31 mshambuliaji Mnyarwanda wa Simba SC, Meddie Kagere alipiga tik-tak nzuri kuunganisha krosi ya beki wa kulia, Zana Coulibally kutoka Burkina Faso, lakini mpira ukagonga mwamba na kurudi uwanjani kabla ya kuondoshwa kwenye eneo la hatari.
    Nahodha, Bocco akaikosesha timu yake bao la wazi dakika ya 48 baada ya kupiga nje akiwa anatazamana na kipa Muivory Coast, Sylvain Gbohouo kufuatia pasi nzuri ya kiungo Mnyarwanda, Haruna Hakizimana Fadhil Niyonzima.
    Bocco tena dakika ya 53 akapiga mpira ukambabatiza kipa na kutoka nje baada ya kupewa pasi nzuri na kiungo Mzambia, Clatous Chama.
    Bocco akakamilisha siku yake mbaya Aprili 6 kwa kukosa penalti dakika ya 59 baada ya shuti lake kupaa juu ya lango kufuatia beki Muivory Coast, Koffi Christian kuunawa mpira uliopigwa na Kagere akiwa nje kidogo ya boksi kulia.
    Kwa Mazembe, wao walitengeneza nafasi mbili tu Aprili 6 za kusema walikaribia kupata bao, zaidi ya hapo waliutawala tu mchezo.
    Kwanza dakika ya nne mshambuliaji wake, Mkongo Jackson Muleka alipoangushwa na kwenye eneo la hatari la Simba SC, lakini refa Mustapha Ghorbal kutoka Algeria akamuonyesha kadi ya njano akidhani alijiangusha – pale asingeanguka kama angepiga ingekuwa habari nyingine.
    Nafasi nyingine nzuri mno Mazembe walipata dakika ya 89, baada ya mtokea benchi Glody Likonza kupiga shuti lililogonga mwamba wa kulia na kutoka nje akiwa amebaki yeye na kipa, Aishi Salum Manula.
    Zaidi ya hapo refa Mustapha Ghorbal alimaliza mpira wakati Mazembe wanajiandaa kupiga kona kutoka upande wa kulia wa Uwanja.
    TP Mazembe imeepuka kurudia makosa ya mwaka jana ilipotolewa katika hatua kama hii na C.D. Primeiro de Agosto ya Angola kwa mabao ya ugenini, baada ya kuanza na sare ya 0-0 Luanda na kwenda kutoa sare ya 1-1 Lubumbashi.
    Pamoja na kutolewa, Simba SC imeiletea faida kubwa Tanzania katika nafasi za ushiriki wake kwenye michuano ya klabu barani, kwani kuanzia msimu wa 2020 -21 itakuwa inapeleka timu nne, mbili Kombe la Shirikisho na mbili Ligi ya Mabingwa.
    Iliwachukua Yanga SC miaka mitatu kukusanya pointi tatu baada ya kuingia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho 2016 na 2018, wakati Simba SC kwa kufika Robo Fainali imekusanya pointi 15 na kufikisha 18 hivyo kuipandisha Tanzania chati hadi nafasi ya 12 tanzania kwenye renki za CAF.
    Pamoja na kutolewa, Simba SC inastahili pongezi kubwa na za dhati, kwani ingeichukua Tanzania muda mrefu kufikia mafanikio hayo. Kwa sasa Simba SC wanatakiwa kwenda kufanyia kazi mapungufu yaliyoonekana kwenye timu, ili msimu ujao wawe katika kiwango bora zaidi waweze kufika mbali zaidi.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: HONGERA SIMBA SC, KAFANYIENI KAZI MAPUNGUFU YALIYOONEKANA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top